Vipigo vyazibeba Simba, Yanga Dar

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa Simba na Yanga walipoteza michezo ya kwanza ya hatua ya makundi ugenini. Simba iliyopo Ligi ya mabingwa Afrika ilifungwa bao 1-0, dhidi ya Horoya kule Guinea wakati Yanga ilikubali kulala kwa bao 1-0, na US Monastir ya Tunisia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

Kufungwa haikuwa habari njema kwa wawakilishi wetu, lakini jambo zuri ni kwamba vinara wa kila kundi ndio tunaowakaribisha nyumbani leo na kesho na hiyo ni faida kwa timu za Simba na Yanga.

Simba iliyopo Ligi ya Mabingwa Afrika ipo nafasi ya tatu na haina pointi wakati Yanga inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika ipo nafasi ya nne na haina pointi.

Kwenye mechi za wikiendi hii kila mmoja anahitaji ushindi kwani utakuwa na maana kubwa tofauti wakipata matokeo ya kufungwa, suluhu au sare.


SIMBA

Simba iliyopo kundi ‘C’ inacheza nyumbani dhidi ya Raja Casablanca na inahitaji ushindi ili kupata pointi tatu za kwanza kwani ikishindwa kufanya hivyo kwa kufungwa au sare pointi moja itawaweka kwenye mazingira magumu.

Kama Simba ikishinda maana yake itakuwa imepata pointi tatu wakati huo itakuwa sawa na vinara wa kundi Raja itakayokuwa imekosa pointi kama itafungwa hapa Dar es Salaam.

Wakati huo Simba itakuwa inasikilizia matokeo ya mchezo mwingine pale Kampala, Uganda kati ya wenyeji Vipers inayoburuza kundi dhidi ya Horoya AC yenye pointi tatu katika nafasi ya pili. Raja ilianza kwa kuipasua Vipers mabao 5-0 kule Morocco.

Kushinda kwa Simba itakuwa pointi sawa na Raja, wakati huo Vipers ikishinda nyumbani kundi litakuwa na timu nne zenye pointi tatu ila kama mechi ikiisha kwa sare Horoya itakuwa kinara kwa kufikisha pointi nne.

Kama Simba itashinda dhidi ya Raja, itakwenda kucheza mechi inayofuata ugenini dhidi ya Vipers ikiwa kwenye hali nzuri japo ikipata sare au hata ikipoteza mchezo wa leo bado atakuwa kwenye kuwania nafasi ya kufuzu robo fainali.

Kwa desturi ya mashindano haya ya Afrika ni muhimu sana kila timu kushinda mechi zake tatu za nyumbani ili kuvuna pointi tisa na kuweka mazingira mazuri ili ikitokea ugenini imepatikana pointi moja au tatu uwe na uhakika wa kufuzu hatua ya robo fainali.

Kwahiyo ushindi wa Simba dhidi ya Raja una maana kubwa kwani itakuwa kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele ila ikiwa tofauti na hivyo itakuwa kwenye wakati mgumu wa kusonga mbele kwani ni mara chache timu kupata ushindi ugenini haswa kuanzia hatua hii ya makundi.

Ukiangalia rekodi za hivi karibuni Simba imepata ushindi katika michezo mingi ya mashindano ya CAF, inapokuwa nyumbani ila kuna michache ilishindwa kufanya hivyo kama dhidi ya Jwaneng Galaxy, UD Songo, TP Mazembe na Al Masry.


YANGA

Kama watani wao, Simba, kwa kupoteza ugenini Yanga wanahitaji kushinda mechi ya nyumbani kesho dhidi ya TP Mazembe inayoongoza kundi ‘D’.

Yanga kama ikishinda maana yake itakuwa pointi sawa na vinara wa kundi TP Mazembe ila hapo itaangaliwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani wageni mchezo wa kwanza ilishinda mabao 3-1.

Kama Yanga ikiweza kuvuna pointi tatu nyumbani itakuwa inasikilizia matokeo ya mchezo wa Real Bamako itakayokuwa nyumbani dhidi ya US Mosastir iliyoshinda mchezo wa kwanza.

Kama Real Bamako itashinda nyumbani maana timu zote zitakuwa na pointi tatu zitaangaliwa zile zenye mabao mengi ya kufunga ndio zitakuwa kileleni mwa msimamo.

Kama Monastir itapata sare ugenini au kushinda maana yake itakwenda kuongeza kundi huku matokeo ya Yanga iliyo mkiani kama itashinda inaweza kuamua kumuweka nafasi ya pili au tatu kwenye msimamo.

Yanga kama itashindwa kupata ushindi nyumbani kesho itajiweka kwenye wakati mgumu wa kusonga hatua inayofuata na itakwenda Mali kucheza na Real Bamako huku morali ikiwa chiini tofauti na kama itashinda.

Ukiangalia rekodi za Yanga kwa kipindi cha hivi karibuni kwenye mechi za nyumbani kama dhidi ya Club Africain, Al Hilal na Rivers United imeshindwa kufanya vizuri kwa maana ya kupata ushindi.

Kwa maana hiyo Yanga inahitaji ushindi wa nyumbani licha ya kucheza dhidi ya timu ngumu Afrika TP Mazembe iliyochukua ubingwa wa mashindano ya CAF, mara tano kwenye vipindi tofauti.


WASIKIE WADAU

Mchezaji wa zamani Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema Yanga kikubwa wanatakiwa kubadilisha aina ya uchezaji na mbinu walizotumia kule ugenini ziwe tofauti na mchezo wa nyumbani.

“Yanga inahitaji ushindi kwanza, inatakiwa kuwa na nidhamu kwenye kuzuia ila muda mwingi icheze kwa kushambulia ili kupata mabao mapema,” alisema SMG.

Mchezaji wa zamani Simba, Abdallah Kibadeni anasema Simba tayari mioyoni kwao huwa na kitu kwamba na matumaini makubwa ya kushinda michezo ya nyumbani, jambo hilo ni zuri ila wachezaji wanatakiwa kuwa na tahadhari.

“Wachezaji wa Simba wanatakiwa kufahamu wanacheza na timu yenye uwezo, sio ya kuibeza, hivyo nidhamu yao na wingi wa mashabiki wao vinaweza kuongeza morali na kuendeleza rekodi ya kufanya vizuri nyumbani,” anasema Kibadeni na kuongeza;

“Yanga katika kipindi cha hivi karibuni haina muendelezo wa matokeo mazuri nyumbani kwa maana hiyo wachezaji wale wapya na uzoefu wa waliokuwa kwenye kikosi wanatakiwa kuonyesha ubora wao ili timu ifanye vizuri.

“Wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wa Yanga wanatakiwa kufahamu wanakwenda kucheza na timu kubwa Afrika na bora kwenye mashindano hayo, nimewatahadharisha hili sababu kuna wengine wanaiona TP Mazembe kama imeshuka ubora vile.”