Prime
Uchaguzi TFF wapingwa BMT

Muktasari:
- Wagombea sita wa nafasi ya urais akiwamo anayetetea kiti, Wallace Karia walifanyiwa usaili huo jana kuanzia saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa moja ya hoteli zilizopo jijini Dar es Salaam, huku gumzo likiendelea kuwa ni ishu ya endorsement ambayo huenda ikawatoa baadhi ya wagombea hao.
WAKATI usaili wa wagombea 25 waliojitokeza kuwania nafasi za kuliongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ukifanyika jana uchaguzi huo umepingwa katika ofisi za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) baada ya mawakili watano kuandika barua ya kutaka usifanyike kwa madai ya kukiukwa kwa taratibu.
Wagombea sita wa nafasi ya urais akiwamo anayetetea kiti, Wallace Karia walifanyiwa usaili huo jana kuanzia saa 4 asubuhi kwenye ukumbi wa moja ya hoteli zilizopo jijini Dar es Salaam, huku gumzo likiendelea kuwa ni ishu ya endorsement ambayo huenda ikawatoa baadhi ya wagombea hao.
Mbali na Karia wengine wanaowania urais ni pamoja na nyota wa zamani wa kimataifa, Ally Mayay, kocha maarufu na mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Dk Mshindo Msolla, Ally Thabit Mbingo, Injinia Mustapha Himba na Shija Richard, huku wagombea 19 wamejitokeza kuomba nafasi sita za ujumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho hilo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 16, jijini Tanga.
Katika usajili huo, Mwanaspoti lilishuhudia Dk Msolla akiwa wa kwanza kutoka katika chumba kilichotumika kwa zoezi hilo na hadi saa 8 mchana wagombea wote sita akiwamo Karia walishasailiwa na zoezi lilihamia kwa wagombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Wagombea wawili walioomba kuhifadhiwa majina yao, walizungumza na Mwanaspoti baada ya kutoka kwenye chumba cha usaili na kudokeza wametimiza wajibu wa kusailiwa na kilichobaki ni suala la kamati kwa ishu ya endorsement kwani wao ni kati ya waliokosa udhamini kwa mujibu wa Ibara ya 10 (3-4) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF ya 2021.
“Usaili umefanyika kama unavyoona tumetoka, kitu kigumu ni ishu ya uthibitishwaji, wameniuliza kwa nini huna nimewajibu, tumebishana kidogo, lakini kama unavyojua wao ndio wenye uamuzi nimewaachia wafanye uamuzi,” alisema mmoja ya wagombea hao, huku mwingine wa nafasi ya ujumbe alisema, alijikuta anapambana na kamati kutokana na utaratibu wa upatikanaji wa endorsement.
“Nimebishana nao sana juu ya uthibitishwaji nimewaambia utaratibu ni kama umewanufaisha waliokuwa madarakani na wanaotetea nafasi zao,” alisema mgombea huyo.
“Sisi tunaogombea sasa ndio wote tunalia na uthibitishwaji, lakini ukiangalia wanaotetea nafasi zao wanajiamini kwa kuwa mfumo unawabeba, unaweza kuangalia tupo kwenye uchaguzi wa kitaifa, lakini leo waziri na wagombea wengine wote wana haki sawa.”
Mbali na hilo la endorsement, Mwanaspoti limedokezwa kuwa pia wapo wagombea watakatwa kutokana na makosa mbalimbali ya ujazwaji wa fomu za kugombea.
“Wanalalamika basi tu, mtu anajaza fomu anashindwa hata kuweka saini yake vizuri, wengine wanashindwa hata kusoma vizuri sehemu walitakiwa kujaza kwa herufi kubwa wameweka ndogo kwa hiyo mambo ni mengi,” alisema mmoja wa wajumbe wa Kamati ya uchaguzi.
Wagombea 19 wa nafasi za ujumbe ni pamoja na; Ally Msigwa, CPA Hossea Lugano, Cyprian Kuyava, Dk David Msuya, Yono Kevela, Evance Mgeusa, Issa Bukuku, James Mhagama, Martin Sekisasa, Juvenalius Rugambwa, Khalid Mohammed, Lameck Nyambaya, Juma Maanya, Mohamed Aden, Robert Kajuba, Rocky Mgeju, Saleh Alawi, Salum Kulunge na Vedastus Lufano.
WAPINGWA BMT
Katika hatua nyingine mawakili watano wa kampuni ya Haki Kwanza Advocates, chini ya Wakili msomi Aloyce Komba, imeandika barua kwa Msajili wa Vyama, Mashirikisho, Taasisi za Michezo, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuzuia mchakato wa uchaguzi huo kwa kukiukwa kwa taratibu.
Katika barua hiyo inalalamikia kukiukwa kwa katiba, sheria, kanuni na sera za michezo nchini na kuomba ofisi ya msajili kuingilia kati na ione haja ya kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo ulioanza Juni 14 na kuhitimishwa Agosti 16 wajumbe watakapopiga kura katika Mkutano wa Uchaguzi.
Mawakili hao watano walioandika barua hiyo kwenda BMT ni Alloyce Komba, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya, Denice Tumaini na Deusdedit D.M. Luteja, ambao ni washirika wa Haki Kwanza Advocates katika utetezi wa haki za wanamichezo na ni sehemu ya wadau wengine wa michezo pia.
Katika narua yao wameainisha kasoro hizo zilizoanishwa ni kukiuka misingi ya uongozi wa Vyama vya Michezo uliowekwa na Sera ya Michezo ya mwaka 1995, bali Katiba na Kanuni hizo ni kinyume na Kanuni za Usajili wa Vyama vya Michezo (GN No. 422/1999), sheria ambazo zinaunda na kusimamia Baraza la Michezo Tanzania ya mwaka 1967 (RE 1971) na Katiba ya Muungano ya Tanzania ya 1977.
Katika malalamiko hayo (a), Mawakili hao wamesema ibara ya 30(4) ya Katiba ya TFF, inamtaka mgombea wa nafasi ya Rais wa Shirikisho hilo aungwe mkono (Endorsed) kwa barua angalau ya wanachama watano.
pamoja na kuainisha dosari zote mawakili hao wameainisha mapendekezo yao kwa BMT ili kuzuia uchaguzi huo, ikiwamo kutumia usimamizi na ulezi vya taasisi za michezo kulielekeza TFF kusimamisha mchakato wa uchaguzi kwa muda kupisha urekebishaji wa dosari zilizoainishwa.
Kuliagiza shirikisho lifanya marekebisho ya Ibara ya 30(4) ya katiba yake na kuondoa sharti la wanachama kuunga mkono (Endorse) mgombea mmoja tu, kwani kuondolewa kutaleta haki na fursa sawa kwa wanafamilia wa mpira na uongozi wa TFF.
Baraza liiagize TFF lifanya marekebisho ya Ibara ya 37(4) ya katiba yake ili kurejesha ukomo wa uongozi kuwa wa vipindi viwili kama ilivyokuwa awali na kwa mujibu wa sera ya Taifa ya Michezo ya mwaka 1995.
Baraza liiagize TFF kuwasilisha kwake kanuni za uchaguzi kwa ajili ya kuzipitia na kuzithibitisha ili zianze kutumika katika uchaguzi wake wa mwaka huu 2025.
Baraza liahirishe Uchaguzi wa TFF wa mwaka huu wa 2025 hadi hapo shirikisho hilo litakapotekeleza maelekezo ya Baraza, mchakato wa uchaguzi huo unaendelea kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi huo.