Ibenge amrudisha Mukoko Congo

Muktasari:

Mukoko amejumuishwa katika orodha ya wachezaji 44 kujiandaa na michezo miwili ya Gabon na Gambia.

Kiungo mkabaji wa Yanga Mukoko Tonombe ameitwa katika kikosi cha Taifa lake cha DR Congo kinachojiandaa na michezo miwili ya kuwania kucheza Fainali za Mataifa Afrika.

Mukoko ameitwa katika orodha ya wachezaji 44 ambao watachujwa na kupatikana 23 watakaounda kikosi kitakachocheza mechi mbili dhidi ya Gabon na baadaye Gambia.

Awali Mukoko aliwahi kuichezea timu hiyo akiwa na kikosi chake cha zamani cha AS Vita lakini atue Yanga hakuwahi kuitwa mpaka sasa kocha wake wa zamani Florent Ibenge amemrudisha tena.

Kiungo huyo anakuwa mchezaji wa pili kuitwa katika timu hiyo akitanguliwa na aliyekuwa mshambuliaji wa Yanga Heritier Makambo ambaye hata hivyo hakufanikiwa kupenya na kuingia katika orodha ya mwisho.


Mtihani mkubwa kwa Mukoko ni kupenya katika orodha ya mwisho ya wachezaji 23 ambapo rekodi inaonyesha asilimia kubwa nafasi kubwa hupenya wachezaji wanaocheza nje ya Taifa hilo hasa kutoka Ulaya.

Tangu atue Yanga Mukoko amekuwa katika kiwango bora akiipa utulivu mkubwa timu yake eneo la kiungo la timu hiyo huku pia akisaidia kufunga akiwa na mabao mawili kwenye Ligi Kuu.

Tangu atue Yanga Mukoko hajawahi kukosa mchezo wowote wa ligi nafasi ambayo imempa ubora mkubwa wa kuongeza ubora wake katika kumudu majukumu ya ukabaji kwenye safu ya kiungo ya Yanga.