Vigogo Simba waamua mazito, Mugalu, Wawa kitanzini

HIZI ni hesabu kali. Kile kikao kizito cha Simba kimetoka na uamuzi mzito wenye nia ya kuhakikisha Simba inatwaa ndoo ya tano ya Ligi Kuu Bara kibabe kabisa.
Asubuhi ya jana, mabosi watano wenye uamuzi ndani ya Simba walifanya kikao kilichochukua saa 2 kukamilika kikianza saa 3:00 hadi saa 5:00 asubuhi nyumbani kwa Kigogo mmoja mzito.
Mwanaspoti linafahamu kwenye kikao hicho walikuwepo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kassim Dewji na Mjumbe wa kamati hiyo, Crescentius Magori pamoja na kocha mkuu, Pablo Franco aliyekuwa na jukumu kubwa la kuzungumzia masuala ya kiufundi.
Kwenye kikao hicho kizito kilichofanyika kwa usiri mkubwa kuna mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwamo ripoti ya usajili wa dirisha dogo, pamoja na mambo mengine yote ya msingi ambayo Pablo ameyaona tangu alipojiunga na Simba.
Inaelezwa kwenye kikao hicho wamekubaliana kuachana na wachezaji wanne kutokana na sababu mbalimbali wakati huo huo wameridhia kuleta mashine nyingine mpya kutoka nje ya Tanzania.
Wachezaji waliokalia kuti kavu ndani ya kikao hicho na muda wowote Simba wanaweza kutangaza kuachana nao ni Pape Ousmane Sakho na Duncun Nyoni waliosajiliwa kwenye dirisha kubwa la usajili kabla ya msimu huu kuanza lakini wame-shindwa kuonyesha makali yao.
Wengine Taddeo Lwanga na sababu kubwa inaelezwa kuachwa kwake ni kutokana na uwepo wa majeraha ya muda mrefu huku Chriss Mugalu naye akiingia katika orodha hiyo kutokana na kushindwa kurudi katika ubora pamoja na majeraha ya mara kwa mara yanayomsumbua.
Beki wa kati Pascal Wawa naye yumo katika orodha ya wachezaji ambao wanaweza kuachwa lakini kwa kipengele kimoja kama Simba katika dirisha hili watapata beki mwingine wa kati mwenye uwezo, tofauti na hivyo au likishindikana hilo ataendelea kubaki hadi mwisho wa msimu.
Majina ya wachezaji wapya waliokubaliana kuwaleta Clatous Chama ambaye Simba wamemalizana naye kila kitu ila kinachosubiriwa ni ruhusa tu kutoka katika klabu yake.
Wengine ni kiungo mkata umeme wa Kibrazil Gerson Fraga ambaye ataanza kucheza kombe la Mapinduzi, winga wa Kabwe Worrios, Harrison Mwendwa na straika mmoja matata kabisa.