Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usisumbuke ! hizi ni njia za kutibu maumivu ya shingo

Muktasari:

Chanzo kikubwa cha kujitokeza kwa tatizo hili ni kujeruhiwa kwa misuli ya shingo pale unapokuwa katika mkao hasi wa kimwili ikiwamo kujipinda kuelekea uelekeo hasi kwa mwili wakati wa mazoezi.

MAUMIVU ya shingo ni moja ya tatizo ambalo wanamichezo na watu wa kawaida limewahi kuwapata katika maisha yao ya kila siku ya mazoezi, tatizo hilo huwa na maumivu ya wastani mpaka makali yasiyovumilika.

Shingo kwa ujumla imeunda na pingili za vifupa vidogo vilivyoanzia katika fuvu la kichwa.

Katikati ya vifupa hivyo huwa na santuri plastiki (cervical disc) ambazo hukaa katikati ya pingili moja na nyingine kazi yake ni kunyonya shinikizo la uzito na kuzuia msagiko.

Vifupa, nyuzi ngumu za ligamenti na misuli ya shingo kazi yake ni kutoa msaada kwa kichwa na kuwezesha miendo mbalimbali ikiwamo juu chini maarufu kama ‘ndiyo hapana’, pembeni na kujizungusha.

Wakati wa mazoezi mbalimbali ya kujenga utimamu wa mwili na afya kwa ujumla mienendo hii inaweza kuleta majeraha madogomadogo yanavyoweza kuleta hitilafu, shambulizi au majeraha ya shingo, hivyo kuleta hisia za maumivu katika eneo hili.

Chanzo kikubwa cha kujitokeza kwa tatizo hili ni kujeruhiwa kwa misuli ya shingo pale unapokuwa katika mkao hasi wa kimwili ikiwamo kujipinda kuelekea uelekeo hasi kwa mwili wakati wa mazoezi.

Vilevile kwa wale ambao ni wafanya mazoezi kwa afya ambao wengi wana kazi zao kama ajira wanaweza kujiongezea kujijeruhi shingo zaidi wakati wa kulala, utumiaji kompyuta, kukaa katika viti vya katika gari, ofisini na nyumbani kwa muda mrefu.

Tatizo hili linaweza pia kuwa ni shambulizi la mifupa pingili za shingo kutokana na kutumika na kulika kwa mifupa hiyo na historia ya kuwahi kupata ajali, magonjwa ya shingo na matatizo ya mishipa ya fahamu.

Mara nyingi watu wazima ndiyo wanaopata tatizo hilo mara kwa mara hii ni kutokana na umri kuwa mkubwa, hivyo kuwa wahanga wa kanuni ya kulika na kutumika kwa viungo vya mwili.

Hutokea mara chache kwa baadhi ya wanaofanya mazoezi wenye dalili ya maumivu ya shingo likawa ni tatizo kubwa, mara nyingi huwa ni maumivu ya kawaida tu yanayoweza kuisha kwa siku chache.

Kwa kawaida maumivu ya kawaida ya shingo huwa yanaweza kuchukua siku 2-5 yakawapotea yenyewe.

Maumivu haya huwa ni kero na yanaweza kuwa makali kwa sababu shingo inapitisha mamia ya mishipa ya fahamu ndio maana huwapo na hisia kali za maumivu.

Maumivu yanaweza kuwa makali kiasi cha kuingilia mwenendo wako wakawaida wa kila siku ikiwamo kushindwa kufanya mazoezi yako ya kila siku.

Yako mambo ya msingi yanayoweza kufanyika nyumbani ili kumsaidia mtu kutatua tatizo hilo au kulipunguza makali mpaka litakapoisha lenyewe.

Ni vizuri kupumzika na kuacha kufanya mazoezi mpaka maumivu yatakapoisha.

Njia rahisi katika siku za awali unaweza kuweka barafu na kuweka kwa dakika 10-15 katika eneo lenye kuuma, barafu iwekwe ndani ya katika mfuko wa kitambaa na unaweza kurudia kadiri ya uwepo wa maumivu.

Baada ya hapo siku za mbeleni unaweza kukanda kwa maji ya moto kwa kutumia kitambaa au mfuko maalumu wa maji moto au kuoga maji ya moto.

Si mbaya kufanya usingaji (massage) au kuchua kwa kutumia mafuta maalumu au kutumia dawa za maumivu za ute mzito za kuchua au zakupulizia.

Vilevile unaweza kutumia dawa za kawaida za maumivu za vidonge kwa ajili ya kukupa utulivu.

Pata mapumziko ya kutosha na hakikisha unasitisha shughuli za kuchokoza maumivu haya ikiwamo kuweka shinikizo kubwa katika shingo.

Epuka kulalia mto mpaka upone, epuka matumizi ya vitu kama kompyuta kwani vinachangia shingo kupinda wakati wa kutumia na vilevile vitu vingine vitakavyosababisha kuinamisha shingo.

Fika katika huduma za afya mapema pale maumivu yasipoisha, yanapokuwa makali yasiyovumilika, yatakapoambatana na homa kali na kuvimba shingo, kufa ganzi au kupoteza hisia maeneo jirani na shingo.