Ushindi IN, Mukoko OUT Yanga

YANGA ipo katika hatua za mwisho kumshusha straika Chico Ushindi anayekuja kufunga usajili wa timu hiyo akitokea TP Mazembe huku Mukoko Tonombe akipelekwa kwa mkopo TP Mazembe.

Yanga inamchukua Ushindi ambaye alikuwa katika hesabu zao kwa muda anatua Yanga kwa mkopo akitokea Mazembe kuja kuziba nafasi ya Yacouba Sogne ambaye bado ni majeruhi.

Dili hilo limekamilika jana baada ya tajiri wa Yanga kufanya mawasiliano na Bilionea wa Mazembe, Moise Katumbi ambaye alikubaliana na uhamisho huo na Mukoko ataondoka leo Jijini Dar es Salaam akiwa na msimamo wake wa kuwachezea miezi sita tu na si vinginevyo.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi wa Mazembe ni kwamba Yanga ilituma mkataba wa Ushindi jana asaini kisha urudishwe haraka kuwahi dirisha la usajili linalofungwa leo usiku.

Hata hivyo, usajili huo wa Ushindi Mazembe umeibana Yanga wakiomba wapewe kiungo Mukoko Tonombe ambaye naye anahamia Lubumbashi kwa mkopo akitokea Yanga licha ya kwamba hakuwa akitaka kwani amepewa dili hilo kwa kushtukiza.

Mukoko amekosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga msimu huu tangu ujio wa viungo wawili Khalid Aucho na Yannick Bangala lakini mmoja wa marafiki zake ameliambia Mwanaspoti kwamba atacheza miezi sita tu Mazembe.

Yanga imeridhia kuondoka kwa Mukoko aliyebakiza miezi sita katika mkataba wake ingawa kiungo huyo Mwanaspoti linafahamu ameumizwa na uamuzi huo akionyesha bado alihitaji kusalia ndani ya klabu hiyo na mazingira ya Tanzania yalishamkolea.

“Tumeshakubaliana kila kitu na Yanga viongozi wetu wa juu wa Mazembe wamekubali kumuachia Ushindi ingawa ni kijana wetu bora hapa aje huko Tanzania kuitumikia Yanga hakuna maneno sasa,” alisema bosi mmoja wa Mazembe jana mchana huku akidokeza kwamba hata wao walikuwa wakifikiria namna ya kumuachia Ushindi kwavile akili yake ilikuwa ikiwaza Yanga tu baada ya kuzungumza na Wakongo wenzie.

Hata hivyo, Yanga italazimika kumshukuru Ushindi katika uhamisho huo baada ya straika huyo anayemudu kutumia miguu yote kulazimisha dili hilo akitishia kugoma kama mabosi wake hawatawapa ushirikiano mabosi wa Yanga katika mazungumzo yao.

“Mchezaji mwenyewe ameonekana kuwa na mapenzi na Yanga, tulishangaa ametufuata na kutuambia Yanga watapiga simu tafadhali tumuachie akacheze kwa kuwa hapa hana uhakika na baada ya muda kweli Yanga wakapiga na wakaongea na bosi Moise (Katumbi).”

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Mukoko ataondoka leo na wiki ijayo atarudi Tanzania kuchukua familia yake tayari kuanza maisha mapya lakini amewaambia rafiki zake ndani ya Yanga kwamba hatasaini mkataba Mazembe zaidi ya miezi sita na punde atarejea kukiwasha Tanzania.

Mwanaspoti ndio lilikuwa gazeti la kwanza kufichua usajili huo wa Ushindi mara baada ya Yanga kuanza mazungumzo naye ingawa baadaye walitaka kughairi.

Mwanaspoti linafahamu tayari straika huyo anayeweza kushambulia akitokea pembeni ameshafanya mazungumzo na kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ambaye ametua jana alfajiri nchini kuendelea na majukumu yake. Wawili hao walizungumza kuhusiana na ishu za kazi na Nabi amefurahia zaidi kukamilika kwa dili hilo.