Usajili mpya Simba utata

UAMUZI wa CAF kuruhusu Simba na Namungo kusajili wachezaji 40 badala ya 30 umewashtua vigogo wa Shirikisho la Soka la Tanzania(TFF) ambao wamelazimika kukutana faragha.
CAF imeziruhusu klabu zote zinazoshiriki mashindano yake msimu huu kusajili wachezaji 40 badala ya 30 kama ilivyokuwa mwanzo, licha ya kwamba uamuzi huo unakinzana na kanuni za Ligi ya Tanzania Bara.
CAF ilitangaza uamuzi huo Jumatano wiki hii ikiwa ni kati ya hatua za kuhakikisha klabu hazikosi idadi ya kutosha ya wachezaji wanaohitajika kwa mechi katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na janga la corona.
“Kamati ya dharura ya CAF imeruhusu timu zinazoshiriki mashindano ya CAF kuwa na idadi ya kutosha ya wachezaji kushiriki katika mechi na imeamua kutumia pendekezo la kamati ya maandalizi ya Afcon kwa maamuzi yafuatayo:
“Kwa mashindano ambayo kanuni imeweka ukomo wa idadi ya wachezaji kama vile yale ya klabu na ya kuwania kombe, kuongeza idadi ya wachezaji 10. Kwa mfano kama kanuni imeweka ukomo wa idadi kuwa ni wachezaji 30, namba itaongezeka kufikia 40.
Kwa mashindano ambayo yanaruhusu kufanya marekebisho ya idadi kutoka mechi moja hadi nyingine kama vile yale ya kufuzu, chama kinaweza kusafirisha bila kikomo idadi ya wachezaji ambayo itawaruhusu kuziba nafasi za wale watakaobainika kuwa na Virusi vya Corona,” ilisomeka taarifa hiyo ya CAF.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ili mchezaji aruhusiwe kucheza mashindano hayo anatakiwa awe na leseni ya kushiriki Ligi ya Ndani katika nchi ambayo klabu husika inatoka.
“Mchezaji anayefuzu kucheza katika Ligi ya Mabingwa Afrika anapaswa kuwa na leseni iliyotolewa na shirikisho au chama cha soka cha nchi husika, amiliki leseni ya CAF, awe amefuzu kushiriki ligi ya ndani ya nchi husika na awe anaishi katika nchi ambayo klabu anayoichezea ipo,” inafafanua ibara ya pili ya kanuni ya tano ya mashindano hayo.
Hata hivyo, ikiwa Simba na Namungo zitaamua kusajili zaidi ya wachezaji 30, kama 10 wa ziada watajiunga nazo kutoka timu nyingine huenda kukawa na ugumu katika kupewa leseni za ndani ambazo ni kigezo kimojawapo cha kufuzu kucheza mashindano ya klabu Afrika kwani kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara hazitoi mwanya huo wa kusajili zaidi ya wachezaji 30.
“Katika dirisha dogo lolote la usajili klabu inayoruhusiwa kusajili mchezaji ni ile ambayo haijatimiza idadi ya mwisho ya wachezaji 30 au ambayo imehamisha mchezaji kwenda klabu nyingine ya ndani au nje ya nchi. Au iliyositisha/kumalizika mkataba wa mchezaji,” inafafanua kanuni ya 63 ibara ya 11.
Lakini kama haitoshi, kanuni za Ligi Kuu zimeweka ukomo wa wachezaji wa kigeni wanaopaswa kusajiliwa na kupewa leseni kwa kila klabu kutozidi 10 jambo ambalo litainyima fursa Simba ambayo hadi sasa imetimiza idadi hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Masoko ya TFF, Boniface Wambura alisema kutokana na muongozo huo wa CAF, kamati ya Sheria na Hadhi ya Shirikisho hilo itakutana ili ione muafaka wa kuzisaidia Simba na Namungo.
“Siku zote kanuni inapotoka katika chombo cha juu inakuwa ‘superior’ (ina nguvu) zaidi ya kanuni za chombo cha chini hivyo kwa muongozo huo wa CAF, Kamati ya Sheria na Hadhi itakutana kuona ni kwa namna gani kanuni hiyo ya CAF inaingiliana na kanuni zetu.
Hata hivyo, ifahamike kuwa kuna leseni ambazo zinatolewa kwa wachezaji wa vikosi vya vijana vya timu ambazo zinawafanya wafuzu kushiriki mashindano ya klabu Afrika,” alisema Wambura.
Ikiwa wawakilishi hao wa Tanzania watabanwa na kanuni za ligi ya ndani, Simba ndio wanaweza kuathirika zaidi kutokana na mahitaji waliyonayo na aina ya wachezaji wanaopaswa kuwanasa ili kutatua udhaifu wao.
Kwa namna Simba ilivyocheza msimu huu, timu hiyo imeonekana kuhitaji kuimarisa nafasi ya beki wa kati kwa kusajili angalau beki mmoja wa kati wa kimataifa pamoja na kiungo mkabaji ambao kiuhalisia wanapaswa kuwa wa kigeni wenye daraja la kuhimili mahitaji ya mashindano hayo.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema; “Sisi kwa sasa hatuwezi kusema wala kuamua lolote hadi pale TFF itakapotupa muongozo wa nini cha kufanya. Wakishatupa maelekzo tutakaa chini kuona tunafanyaje.”
Try Again aliongeza kwamba watalazimika kukutana na Sven kwa haraka kuangalia kama kuna ulazima wa kusajili mastaa wengine wa kigeni kwa ajili ya ushiriki wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambako wataiwakilisha Tanzania.
ISHU YA MUKOKO
Simba wamekuwa wakiwarusha roho Yanga kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanamchukua staa wao, Mukoko Tonombe ingawa hakuna yoyote aliyethubutu kujitokeza hadharani na kufafanua sakata la mchezaji huyo mwenye mkataba wa miaka miwili na Yanga.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hersi Said amesisitiza kwamba Mukoko ni mali ya Yanga kwa miaka mingine miwili ijayo kwavile amesaini mkataba huo hivi karibuni mbele ya viongozi wa timu yake ya zamani ya AS Vita.
Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Yanga imemnunua Mukoko kama ilivyo mwenzie Tuisila Kisinda kwa zaidi ya Sh300milioni.
Meneja wa Mukoko, Nestor Mutuale aliiambia Mwanaspoti jana kwamba; “Kama Simba wanamtaka Mukoko wazungumze na Yanga.” Lakini mmoja wa viongozi wa juu wa Simba alicheka na kusisitiza kwamba ni mambo ya mitandaoni wao hawana ishu na Mukoko.