USAJILI MPYA SIMBA NOMA

Muktasari:
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara tayari wamefuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA huku wakiongoza msimamo wa ligi kwa pointi 55 wakati zikiwa zimebaki mechi sita tu, jambo ambalo linawaweka karibu na mashindano hayo ya kimataifa mwakani.
SIMBA sasa imetega macho yake katika tiketi mbili za mashindano ya kimataifa ambazo zipo mbele yao na ikitokea tu wakajihakikishia ushiriki wa mashindano hayo, watafanya usajili kabambe.
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara tayari wamefuzu hatua ya nusu fainali ya Kombe la FA huku wakiongoza msimamo wa ligi kwa pointi 55 wakati zikiwa zimebaki mechi sita tu, jambo ambalo linawaweka karibu na mashindano hayo ya kimataifa mwakani.
Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange Kaburu alisema kama watapata tiketi ya uwakilishi katika michuano ya kimataifa watahakikisha wanakisuka kikosi chao vilivyo ili wawe na timu ya ushindani mkubwa.
Kaburu alisema hawataki kwenda kupata aibu katika mashindano hayo ya kimataifa na kuishia hatua za awali, hivyo ni lazima wawe na kikosi kipana ambacho kitawawezesha kufika angalau hatua ya makundi.
“Usajili wetu kwa sasa tumeusimamisha ili kuona tunapata tiketi gani ya uwakilishi wa mashindano ya kimataifa. Tayari tupo karibu na hilo, baada ya kupata tiketi ndipo tutafahamu tunahitaji kikosi cha aina gani,” alisema Kaburu.
“Kama tutakwenda katika mashindano hayo ya Afrika, ina maana kwamba tutahitaji kuwa na kikosi kipana zaidi. Tutasajili kwa akili ya mashindano hayo ili tukienda tuweze kufanya vizuri zaidi.”
Akimzungumzia staa wao Mbaraka Yusuf anayecheza kwa mkopo Kagera Sugar, Kaburu alisema watafanya tathimini baada ya msimu kumalizika ili kuona kama anaweza kuwa msaada kwao katika mashindano yanayokuja.
“Ni kweli mkataba wake unamalizika, tunasubiri kuona tunakwenda katika mashindano gani mwakani. Kocha atasema kama atamwitaji ama la. Wapo pia wachezaji wengine wa mkopo, tutatazama kama tunaweza kuwarejesha,” alisema.
Mwanaspoti linajua kwamba wachezaji wapya ambao wako kwenye listi ya Simba ni Emmanuel Okwi wa Uganda, Kenny Ally wa Mbeya City, Awesu Awesu wa Madini FC na Mbaraka aliyeko Kagera.
MGOSI KASEMA
Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema wanawategemea nyota ambao walikuwa kwenye majukumu ya Taifa Stars, kurejea na mbinu mpya kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo kwenye harakati za kuwania ubingwa.
Nyota wa Simba ambao walijumuishwa kwenye kikosi cha Stars ni Ibrahim Ajib, Mzamiru Yasini, Abdi Banda, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Shiza Kichuya na ndiyo wanaunda kikosi cha kwanza cha Wana Msimbazi.
“Ukizingatia Simba, hatukuwa na michuano ya kimataifa ndani ya miaka minne, hivyo tunatarajia waliobahatika kwenda kulitumikia taifa watarejea na vitu vipya walivyojifunza huko kwa manufaa ya timu,” alisema.
Aliongeza: “Cha msingi ni kuona kwamba wachezaji wetu tunaowategemea walipata nafasi ndani ya kikosi cha Stars, kilichopo chini ya kocha Salum Mayanga hivyo ujuzi wao utakuwa msaada katika mechi sita zilizosalia.”
Alimzungumzia Laudit Mavugo kwamba licha ya kwamba alikuwa kwenye timu yake ya taifa ya Burundi lakini alionyesha uwezo utakaosaidia kikosi hicho hasa kwenye kupata ushindi.
“Ni kwamba kucheza kwake kulimfanya awe mchezoni hilo ndilo tunaloliangalia kiundani kwamba baada ya kupumzika kwa ligi hatukukaa bure,” alisema.
Mbali na hilo alisema watakuwa na kazi ngumu dhidi ya Kagera Sugar, iliyo chini ya kocha Mecky Maxime kwamba na wao wanapigana kufa, kupona kupata pointi tatu.
Kwa upande wa Mecky alisema hawezi kuipuza Simba, lakini amewajenga kisaikolojia wachezaji wake kuhakikisha wanashinda.
“Si kazi rahisi ukizingatia Simba, wapo kwenye mbio za ubingwa na sisi malengo yetu kumaliza nafasi za juu,” alisema.