Kisa Mbeya City, Prisons yajipanga upyaa

Muktasari:
- Chanzo cha ndani kutoka timu hiyo, kilisema uongozi umeanza na kuweka skauti kila mkoa uliyo na klabu ya Ligi Kuu, ili kusaidia kuwapata wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa.
KUREJEA tena kwa Mbeya City katika Ligi Kuu Bara, kumeizindua Tanzania Prisons kuanza mipango mapema ya kujipanga ikitaka kusajili kikosi imara kitakachotengeneza ushindani wa kuwania nafasi za juu katika msimamo na sio kujikwamua kushuka daraja, kama ilivyopitia katika misimu ya hivi karibuni.
Chanzo cha ndani kutoka timu hiyo, kilisema uongozi umeanza na kuweka skauti kila mkoa uliyo na klabu ya Ligi Kuu, ili kusaidia kuwapata wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa.
“Japo mbele yetu tuna jukumu kubwa la kuhakikisha timu inasalia Ligi Kuu kwa kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Yanga na Singida Black Stars ili tusicheze mtoano, lakini lazima kila kitu kifanyike kwa wakati,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Tukifanikiwa kusalia Ligi Kuu tutakuwa na dabi baina yetu na Mbeya City, hivyo kila upande utahitaji kuwa na wachezaji ambao utawapa furaha mashabiki wake na mechi zetu zinakuwa ngumu kama Simba na Yanga zinapokutana, hivyo lazima tuongeze nguvu katika usajili.”
Chanzo hicho kilisema nje mikoa iliyo na timu za Ligi Kuu pia wameenda mbali kama Uganda na hata Zanzibar pia wana skauti, kitu kikubwa wakihitaji kuirejesha Prisons ya ushindani mkubwa na ngumu kufungika kirahisi.
Prisons ipo nafasi ya 13 katika mechi 28 imeshinda nane, sare sita, imefungwa mechi 14, imefungwa mabao 38, imefunga mabao 23 ina pointi 30.