Refa wa kwanza mweusi EPL, Uriah Rennie afariki dunia

Muktasari:
- Rennie alichezesha zaidi ya michezo 300 kati ya mwaka 1997 na 2008, ikijumuisha mechi 175 za EPL.
LONDON, ENGLAND: Mwamuzi wa kwanza mwenye asili la Afrika aliyechezesha Ligi Kuu ya England (EPL), Uriah Rennie, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 65.
Rennie alichezesha zaidi ya michezo 300 kati ya mwaka 1997 na 2008, ikijumuisha mechi 175 za EPL.
Chama cha Soka cha Kaunti ya Sheffield & Hallamshire kilithibitisha kifo cha mwamuzi huyo, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa eneo hilo.
"Tuna huzuni kubwa kutangaza kifo cha mwenyekiti wetu wa zamani na mwamuzi wa EPL, Uriah Rennie," ilieleza taarifa hiyo na kuendelea;
"Uriah aliweka historia kama mwamuzi wa kwanza mweusi katika Ligi ya EPL, akichezesha zaidi ya mechi 300 za Ligi Kuu kati ya 1997 na 2008. Alivunja vizuizi, akaunda jumuiya yetu ya soka na kuhamasisha vizazi vijavyo."
Hivi karibuni Rennie alifichua kuwa, alikuwa akifanya mazoezi ya kutembea tena baada ya kuugua ugonjwa wa kupooza.
Mwamuzi huyo mzaliwa wa Jamaica, alihamia Sheffield akiwa na umri mdogo na alianza kujifunza kazi hiyo mwaka 1979 kabla ya kuweka historia 1997 alipochezesha mechi ya EPL kati ya Derby County na Wimbledon.