Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unabisha? Yanga 4 Simba 2

Muktasari:

Kama kocha, kiongozi au mchezaji amefanya vibaya, kuboronga kwenye mchezo huu huwa ni mwanzo wa lawama na shutuma zinazoweza kumfukuzisha mtu kibarua.

ULE muda wa lawama umewadia! Simba na Yanga zinatarajiwa kuvaana wikiendi hii katika pambano la Ligi Kuu Tanzania Bara. Pambano ambalo wadau wa klabu hizo huwa roho juu kwa muda wote wa dakika 90. Pia ndilo pambano ambalo huibua mazuri au mabaya yote yanayowahusu wachezaji, viongozi na makocha.

Kama kocha, kiongozi au mchezaji amefanya vibaya, kuboronga kwenye mchezo huu huwa ni mwanzo wa lawama na shutuma zinazoweza kumfukuzisha mtu kibarua.

kadhalika ni pambano ambalo hufanya kocha, mchezaji au kiongozi goigoi na mwenye shutuma kupapatikiwa. Yaani ni sawa na shetani kugeuzwa kuwa malaika.

Bahati nzuri pambano hili limekuja wakati Simba ikiwa imetoka kuzinduka usingizini na kuwapa presha wapinzani wao wa Ligi Kuu. Kabla ya hapo Simba ilikuwa timu ya kawaida sana. Ilichukuliwa poa na kubezwa kuwa ya ‘mchangani’. Kwa sasa hata wale waliokuwa wakiimba wimbo huo, wameufyata. Wanaanzaanzaje kuibeza wakati ipo kileleni baada ya kushuka uwanjani katika mechi 19? Vilevile mchezo huo wa 96 kwa klabu hizi katika Ligi ya Tanzania, umekuja wakati Yanga ikiwa imetoka kufanya yake anga za kimataifa. Jumamosi iliyopita, licha ya kuwa na uchovu wa safari na kucheza kwenye Uwanja ulioharibiwa na maji ya mvua, ilishinda ugenini bao 1-0 katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

REKODI TAMU

Kwa mujibu wa rekodi za mechi za watani katika misimu mitano iliyopita kuanzia 2010-2011, Simba na Yanga zimekutana mara 11. Katika mechi hizo Yanga ndio vijogoo mbele ya Simba kwani imeshinda mara nne, huku wenzao wakishinda mara mbili tu.

Timu hizo zimetoka sare mara nne pia na zote zikiwa zimefunga idadi sawa ya mabao kila moja ikiwa na mabao 12. Mabao hayo yanajumuisha na mchezo wa duru la kwanza lililochezwa Septemba 26, mwaka jana na Simba kulala mabao 2-0. Yanga imefanikiwa kukusanya jumla ya pointi 17 dhidi ya 10 za wapinzani wao.

Katika rekodi hizo, Simba licha ya kupata ushindi mara chache, lakini imeweka rekodi tamu kwa kuifunga Yanga idadi kubwa ya mabao katika pambano lao la Mei 6, 2012 wakifungia msimu wa 2011-2012 ambao Simba ilinyakua taji lake la mwisho la Ligi Kuu.

Yanga ilikubali kipigo cha mabao 5-0, huku Yanga ushindi wake mkubwa ni ule wa mabao 2-0 iliyopata mara mbili ikiwamo mwaka jana.

Timu hizo pia zimetoka sare yenye idadi kubwa ya mabao Oktoba 20, 2013 pale zilipofungana mabao 3-3. Mechi moja pekee baina yao ndio haikuzaa mabao nayo ilikuwa ni ya Oktoba 18, 2014.

WATUPIAJI

Waganda Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi ndio wachezaji waliofunga idadi kubwa ya mabao ndani ya mechi hizo 11, kila mmoja akiwa na mabao matatu. Kiiza aliyafunga akiwa Yanga na Okwi aliyafunga wakati akiichezea Simba.

Jumla ya wachezaji 20 waliohusika kwenye mabao katika mechi za misimu hiyo yote ni watano tu ndio waliosalia katika timu hizo, huku wengine 15 hawapo ndani ya timu hizo. wachezaji ambao hawapo ni Jerry Tegete, Stephano Mwasyika, Davies Mwape, Said Bahanuzi, Didier Kavumbagu na Mrisho Ngassa waliokuwa Yanga, huku Simba akikosekana Okwi, Patrick Mafisango (marehemu) Juma Kaseja, Felix Sunzu, Amri Kiemba, Betram Mombeki, Joseph Owino, Gilbert Kazze na Haruna Chanongo.

Waliosalia na wanaoweza kuendelea kutupia ni Mussa Mgosi na Kiiza ambaye hata hivyo kwa sasa yupo Msimbazi na si Yanga tena, huku Jangwani wapo Simon Msuva, Amissi Tambwe na Malimi Busungu. Safari hii watatokaje?

HAKUNA KISINGIZIO

Pambano hilo la Jumamosi kwa namna lilivyokuja, bila shaka halitakuwa na visingizio. Yanga wapo vizuri, Simba wamekamilika.

Kocha Jackson Mayanja ameshinda mechi saba mfululizo, sita za Ligi Kuu na moja ya Kombe la FA. Timu inaundwa na vijana wenye damu mchanganyiko na wanaokimbiza kwelikweli, sasa hapo lawana zitoke wapi? Yanga nako kwa msimu wa pili sasa wapo na Kocha Hans Van Pluijm. Ina nyota kadhaa wa kimataifa wenye viwango vya juu. Timu imetulia, wachezaji wamezoeana na wanacheza kitimu kusaka ushindi. Hata kama Wagosi wa Kaya waliwatibulia wiki tatu zilizopita, lakini bado Yanga ipo njema.

Yanga imecheza mechi 18 na kushinda 13, imeambulia sare nne na kupoteza mchezo moja. Si mbaya sana kwani inatofautiana na Simba kwa pointi mbili tu. Simba yenyewe imeshinda mechi 14 katika michezo 19 iliyocheza ikipata sare tatu na kupoteza mbili. Ni lazima zitashuka uwanjani Jumamosi zikiwa na dhamira moja tu ya kutaka kujenga heshima na kujiweka kwenye mazingira mazuri katika ligi hiyo. Wanajua Azam waliopo nafasi ya tatu, hajalala! Kufungwa bao 1-0 na Coastal Union, hakuwezi kuwafanya Wanalambalamba kuzubaa.

UKUTA WA JIWE

Yanga licha ya kutetereka kwa Coastal, bado ndio timu yenye ukuta wa chuma. Timu hiyo imeruhusu mabao tisa tu nyavuni mwao, huku ikifunga jumla ya mabao 42. Ni mabao mengi wakati ligi ikiwa ndio kwanza imeanza mechi za duru la pili. Watani zao Simba nao sio wa kubezwa. Ndio timu ya pili yenye mabao mengi nyuma ya Yanga. Imefunga jumla ya mabao 35 na kufungwa 11. Ukuta wao ndio wa pili kwa kuruhusu mabao machache wakiwa sambamba na Azam, ambayo hata hivyo ina michezo mwili pungufu ikifunga mabao 31 na kufungwa mabao 11 pia.

Kwa mnasaba huo, bila shaka mechi ya Jumamosi itakuwa ni kazi ya kuta za timu hizo kuendeleza rekodi ya kutufungwa kirahisi. Makipa wa timu hizo wasingependa kuingia kwenye lawama, ikizingatiwa mechi hiyo ni ya lawama zaidi ya idhaniwavyo!

FUNGA NIKUFUNGE

Umeuangalia msimamo wa ligi ulivyo, umeona nini? Timu zote zina mabao mengi. Zinafunga kila zinapopata nafasi. Bahati nzuri ni kwamba kila upande una wafungaji. Simba kuna Hamis Kiiza ‘Diego’, Ibrahim Ajib na Danny Lyanga. Wamezitesa sana timu nyingine kwa pilikapilika zao uwanjani. Wamefunga jumla ya mabao 26 kati ya 35. Mabao tisa tu ndio wachezaji wengine wamechangia, Kiiza ana 16 akiongoza orodha ya wafungaji wa ligi hiyo, Ajib ana manane na Lyanga ana mawili. Geukia upande wa pili, Yanga ina wakali kama Amissi Tambwe. Jamaa anajua kufunga. Misimu mitatu ya kuwepo Tanzania amefunga jumla ya mabao 47.

Msimu huu ana mabao 14 akishika nafasi ya pili nyuma ya Kiiza. Mstraika wenzake wawili, Donald Ngoma na Simon Msuva nao wamechangia jumla ya mabao 16. Ngoma ana 10 na Mfungaji Bora wa msimu uliopita, Msuva amefunga sita. Utatu wao umezaa jumla ya mabao 30.

Yanga ina wafungaji wengine kama Thabani Kamusoko, kiungo kutoka Zimbabwe ambaye ana mabao matano mpaka sasa. Pia ina Paul Nonga mwenye mabao manne, aliyohama nayo kutoka Mwadui Shinyanga na Malimi Busungu mwenye mawili.

Kifupi pambano la Jumamosi litakuwa ni funga nikufunge na yeyote atakayezubaa atachekwa Taifa.