Ukiwa na macho ZPL marufuku

Muktasari:

  • Taarifa hiyo ya bodi imepokelewa kwa mitazamo tofauti na klabu. Ofisa Habari wa Uhamiaji FC, Mwinyi Hamad alisema utaratibu huo utakuwa mzuri kwa sababu utawalinda wachezaji wengine kupata maambukizi.

UNGUJA. BODI ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPLB) kupitia kwa Mtendaji Mkuu, Issa Kassim ameliambia Mwanaspoti hawatamruhusu kucheza mechi mchezaji yeyote atakayebainika kuwa na tatizo la macho mekundu maarufu kama red eyes.

“Uzuri haya maradhi hayamfichi mtu mwenye nayo anaonekana wazi wazi  kwahiyo hakuna ulazima wa kubeba vifaa mchezaji ukimuona tu utamjua kama anayo au hana,” alisema Kassim.

Taarifa hiyo ya bodi imepokelewa kwa mitazamo tofauti na klabu. Ofisa Habari wa Uhamiaji FC, Mwinyi Hamad alisema utaratibu huo utakuwa mzuri kwa sababu utawalinda wachezaji wengine kupata maambukizi.

JKU taarifa hiyo haikuwa nzuri kwa upande wao, kwani kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Ali Haji alisema; “Kawaida mchezaji akiumwa haswa hawezi kucheza mechi mwenyewe tu atakaa juu, lakini kama anaweza kucheza basi huyo haumwi, sasa waje uwanjani halafu uwatoe hii sio haki tutakuwa tuna wanyanyapaa jambo ambalo sio sahihi kama anaweza kucheza mechi  aachwe acheze.”

Haji alisema hofu yake kubwa kuona kutatokea hujuma kwa baadhi ya timu kutolewa kwa wachezaji wao kwa makusudi kwa kisingizio cha kuumwa macho kumbe wana mpango wao wa kuirahisishia timu fulani.

Daktari Mkuu wa Zanzibar Heroes na Polisi Zanzibar,  Mohammed Said alisema; “Haya maradhi yanaambukizwa kwa njia mbili ‘direct’ na ‘indirect’, hivyo wachezaji wawe wasafi wanawe uso mara kwa mara waepuke kupeana mikono.”

Alisema ni vyema Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kuweka maji na sabuni kwenye viwanja ambavyo vitatumika kuchezewa ligi, wachezaji wawe wananawa kabla na baada ya mechi.
Kiungo wa Kundemba, Fahmi Salum’ Miguel’ ambaye kwa sasa yupo nje akisumbuliwa na maradhi hayo alisema “Unakuwa huna raha hufanyi mazoezi kwa umakini kwa hiyo unaona bora utulie tu, niwaambie wachezaji wenzangu wawe makini na kila mmoja amkinge mwenzie.”

Mshambuliaji wa KVZ, Chunga Said Zitto ambae naye alipata changamoto hiyo lakini kwa sasa amesharejea, alisema mchezaji hukosa ufanisi wa kucheza kwa sababu jasho likiingia machoni huzidi kuuma hivyo inakuwa mtihani kwao.

Hadi jana wachezaji waliopatwa na ugonjwa huo kwa upande wa timu za Ligi Kuu ambazo zipo Unguja ni 33. Katibu Mkuu wa Kipanga, Maulid Othman alisema wao walichokifanya ni kuwaweka kambi wachezaji wao wote ili kuwanusuru na maradhi hayo jambo ambalo limewasaidia.

Msemaji na Mshauri wa New City yenye maskani yake Dole Wilaya ya Magharibi A Unguja, Idrissa Yakuit, aliliambia Mwanaspoti hawana mchezaji yeyote aliyepata changamoto hiyo hadi sasa.

Mafunzo FC, Kipanga FC, New City na Uhamiaji FC hizi ndio timu ambazo hadi jana hazikuwa na wagonjwa.


TANZANIA BARA
Chama cha Madaktari wa Tiba za Wanamichezo (TASMA), kupitia kwa Katibu wao mkuu, Juma Sufiani alisema licha ya mlipuko huo bado ligi itaendelea japo watoa tahadhari ili kuepusha maambukizo.