Udhamini kitendawili Gor Mahia

Wanandinga wa Gor Mahia wakishangilia uwanjani kwa staili yake hivi karibuni, Mdhamini ni tatizo kwa sasa katika timu hiyo pendwa na watu wengi nchini Kenya.
Muktasari:
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Kenya, huenda wakapoteza udhamini wao mkubwa kutoka katika kampuni hiyo baada ya mkataba wao wa sasa kufika kikomo mwezi ujao.
MWENYEKITI wa klabu ya Gor Mahia, Ambrose Rachier, ameyapuuza madai kwamba klabu hiyo huenda ikapoteza udhamini wake kutoka kwa kampuni ya maziwa Tuzo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Kenya, huenda wakapoteza udhamini wao mkubwa kutoka katika kampuni hiyo baada ya mkataba wao wa sasa kufika kikomo mwezi ujao.
Duru za kuaminika, zinaarifu kuwa kampuni hiyo haiwazi tena kuendelea kuidhamini Gor Mahia baada ya Machi na hivyo kuitaka kuanza kutafuta wadhamini wengine.
“Gor Mahia italazimika kutafuta mfadhili mwingine sababu Tuzo haipo tayari kurefusha mkataba huo, bado hawajawasiliana na klabu rasmi kuhusu hatua hiyo lakini watafanya hivyo hivi karibuni,” mmoja wa maofisa wa karibu wa kampuni huyo amesema.
Julai mwaka jana, Gor Mahia itakayoliwakilisha taifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ilitia sahihi mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini na Tuzo ulioipa klabu hiyo Sh29.5 milioni kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mkataba huo ulikuwa kwa ajili ya malipo ya mishahara ya wachezaji, jezi na shughuli nyinginezo za uendeshaji wa klabu.
Mwaka 2011, Gor na Tuzo walitia saini mkataba wa miaka miwili wa Sh38 milioni ambapo ulimalizika hapo Aprili 2013 kabla ya kuurefusha miezi miwili baadaye.
Mwenyekiti wa Gor, Ambrose Racheir, ambaye hivi majuzi alichaguliwa tena kuongoza kwa muhula wa nne, alisema kwamba hajapokea taarifa zozote kuhusiana na wadhamini hao kutoendeleza mkataba na kuahidi kutoa taarifa baadaye.
“Ikiwa kufikia mwisho wa Machi hawatarefusha mkataba huo nasi basi ndio tutakapokuwa na jambo la kuzungumzia. Kwa wakati huu masuala hayo ni uvumi tu ambayo hatuwezi kuuzungumzia,” Rachier alieleza.
Ikiwa mkataba huo hautaendelezwa kweli, ni wazi klabu hiyo itakuwa imeingia katika hali ngumu kiuchumi inayoweza kuidhoofisha hata katika ushiriki wake kwenye mashindano ya Afrika.