Nenda Aziz Ki hauna deni Tanzania

Muktasari:
- Jamaa wameonyesha jeuri yao ya fedha bwana kwa kumchomoa staa na kipenzi cha Yanga ambaye tayari ameshaondoka Tanzania kwenda Morocco kuungana na miamba ya huko kwa mkataba wa miaka miwili.
MAPEMA tu mwezi ujao hapa kijiweni tutakaa mbele ya runinga kumtazama Stephane Aziz Ki akikiwasha katika Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani akiitumikia Wydad ya Morocco.
Jamaa wameonyesha jeuri yao ya fedha bwana kwa kumchomoa staa na kipenzi cha Yanga ambaye tayari ameshaondoka Tanzania kwenda Morocco kuungana na miamba ya huko kwa mkataba wa miaka miwili.
Kimsingi kwa kauli moja hapa kijiweni tunaiunga mkono Yanga kumuuza Aziz Ki na kiuhalisia anaondoka akiwa hajaacha deni analodai wala analodaiwa kutokana na yale aliyofanya katika kikosi cha timu hiyo ambayo alijiunga nayo mwaka 2022 akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast.
Jamaa kimsingi aliiongezea hadhi ligi yetu na hapana shaka kiwango chake na mchango aliokuwa akitoa utakuwa darasa kubwa kwa wachezaji wetu wazawa katika kipindi hiki ambacho tunatamani kuona wakipandisha viwango vyao na kuwa katika daraja la juu la ubora.
Alikuwa ni mchezaji wa mechi kubwa na zipo nyingi alizoziamua kwa mabao yake hasa ya mashuti yaliyoonekana kuwa mwiba kwa safu za ulinzi za timu mbalimbali za Tanzania na hata zile za nje zilizokutana na Yanga katika mashindano ya kimataifa.
Mfano wa mechi kubwa ambazo Aziz Ki alitamba vilivyo ni dhidi ya watani wa jadi wa Yanga, Simba ambao aliwafunga mara tatu tofauti akiwa na jezi za kijani na njano tena jambo ambalo sio rahisi kwa wachezaji wa kizazi cha sasa kulifanya.
Msimu wa kihistoria ambao Yanga ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Aziz Ki ndiye alianzisha safari yao ya matumaini kwa kufunga bao pekee lililoivusha kuipeleka hatua ya makundi dhidi ya Club Africain ya Tunisia ugenini.
Kawafungia Yanga mabao ya kutosha na msimu uliopita akaweza kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu huku akitwaa tuzo ya mchezaji bora na haikushangaza kuona klabu hiyo ikitoa fedha nyingi kumuongezea mkataba mpya mwaka jana.
Kiufupi Aziz Ki hana baya kwa Yanga na hata soka la Tanzania kiujumla kwani miaka yake ya mkataba kaitumikia vyema na hakuna anayeweza kumlaumu kwa kwenda kutafuta malisho ya kijani zaidi.