Tunawapiga mapemaaaaa!

SIMBA tayari ipo jijini Dodoma kwa mchezo wao wa kiporo cha Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji, huku kila timu ikitamba itamaliza mambo mapema ili kuvuna pointi tatu na nyota wapya wa Msimbazi, Perfect Chikwende na Taddeo Lwanga wataionja ligi kwa mara ya kwanza.
Simba na Dodoma zitavaana kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiwa ni kati ya mechi mbili za viporo zinazochezwa leo, nyingine ikipigwa Dar es Salaam kati ya KMC dhidi ya Namungo itakayopigwa Uwanja wa Uhuru.
Mechi hizo ni mwanzo wa kurejea upya kwa Ligi Kuu iliyosimama kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji Wanaocheza Ardhi ya Nyumbani (Chan) zinazoendelea Cameroon.

Kusimamishwa kwa ligi hiyo kuliwafanya nyota wawili waliosajiliwa Sinmba dirisha dogo, Chikwende na Lwanga kushindwa kuanza kuitumikia, lakini leo wanaweza kuanza dhidi ya Dodoma kabla ya kuliwa kiporo kingine Jumapili Dar es Salaam dhidi ya Azam FC.
Kiwango bora kilichoonyeshwa na wawili hao katika mashindano ya Simba Super Cup yaliyofanyika wiki iliyopita na kile cha Lwanga kwenye Kombe la Mapinduzi, kinatoa ishara kuwa nyota hao watakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoikabili Dodoma, huku wakihitaji ushindi zaidi kwa sababu kuu mbili.

Kwanza ni kupunguza pengo la pointi baina yake na vinara wa ligi, Yanga, libaki pointi sita kwani kwa sasa Simba iko nafasi ya pili ikiwa na pointi 35 wakati Yanga wanaoongoza wana pointi 44, licha ya kutofautiana michezo. Yanga imecheza mechi 18, tatu zaidi ya Simba yenye 15. Kwa vile Simba ina mechi tatu za viporo ili iwe sawa na Yanga kwa idadi ya michezo, ikiwa itapata ushindi na pia katika nyingine mbili dhidi ya Azam na Namungo FC, itafikisha pointi 44 na kukaa kileleni mwa msimamo, kwani itabebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa yenyewe ina utofauti wa mabao 32 hadi sasa wakati Yanga ina wa mabao 22.
Lakini sababu ya pili ni kujiweka sawa kisaikolojia kwa ajili ya mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itaanzia ugenini kuikabili AS Vita Club ya DR Congo, Februari 12.
Kama ilivyo kwa Lwanga na Chikwende ndivyo pia itakuwa kwa Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomez na yule wa makipa, Milton Nienov ambao wamejiunga na Simba hivi karibuni
Ni mchezo ambao Simba wanapaswa kuwa makini zaidi kwa mbinu ya mashambulizi ya kushtukiza ambayo yamekuwa ikitumiwa na Dodoma Jiji hasa inapokuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri ambako wamekuwa wagumu kufungika.
Katika mechi saba ilizocheza Dodoma, timu hiyo imepata ushindi mara tano na kutoka sare michezo miwili.
Simba wanapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji Seif Abdallah Karihe ambaye amekuwa silaha muhimu ya Dodoma Jiji katika mbinu ya kushambulia kwa kushtukiza na hadi sasa ameifungia mabao matano. Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makatta alisema kuwa vijana wake wako tayari kuikabili Simba.
“Ni mechi muhimu kwetu ukizingatia hatupo mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi, hivyo tunahitajika kupata ushindi na wachezaji wangu wanalifahamu hilo,” alisema Makatta.
Kwa upande wa Didier Gomez alisema anaingia katika mechi hiyo akiwa na taarifa za kutosha za wapinzani wao. “Nimewafuatilia kwa ukaribu Dodoma Jiji na nafahamu mengi kuhusu wao. Lakini pia hata kwa timu nyingine na ligi ya hapa Tanzania kiujumla.
“Ni mechi ya ugenini naamini itakuwa ngumu lakini Simba ni timu kubwa na ina uwezo wa kupata ushindi popote - kubwa ni wachezaji kujituma na kufanya kile wanachohitajika kufanya,” alisema Gomez.
KMC, NAMUNGO
Mchezo mwingine unaopigwa jijini Dar, Kocha msaidizi wa KMC, Habib Kondo alisema anakiamini kikosi chake na kwenye mechi ya leo ili kutoka na ushindi dhidi ya Namungo ambayo kupitia kocha wake, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema hana presha yoyote.
Kondo alisema kikosi hicho kimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mtanange huo na hana hofu kwani viongozi na benchi la ufundi limejipanga vyema kuhakikisha alama tatu zinabaki kwao kama wenyeji.
“Ni muda sasa hatujacheza mechi, ukiacha zile za kirafiki ambazo tulikuwa tunacheza, lakini bado timu ipo kwenye ubora wake na kesho tunaingia uwanjani tukiwa na uhakika wa kupata matokeo mazuri, tunajua Namungo ni timu nzuri lakini sisi ni wazuri zaidi yao,” alisema Kondo.
KMC ipo nafasi ya saba baada ya kucheza mechi 17 ikiwa na alama 22, wakati Namungo iko nafasi ya 15 na kocha wake alisema anataka kutumia mechi zao mbili za viporo ukiwamo wa leo dhidi ya KMC na ule wa Ruvu Shooting utakaopigwa Jumapili kujiweka vyema kwa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Namungo itaanzia ugenini kwa kucheza na 1 de Agosto ya Angola, Februari 14 kabla ya kurudiana nayo Azam Complex ili kuwania kutinga makundi.