Chikwende, Lwanga kuonja balaa la Ligi Kuu

Muktasari:
Simba imebakiza mechi tatu za viporo, ila itaanza kwa kucheza na Dodoma Jiji, kabla ya kuivaa Namungo.
Dar es Salaam. Nyota wapya waliosajiliwa na Simba, Perfect Chikwende na Taddeo Lwanga kwa mara ya kwanza wataonja ladha ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakati timu hiyo itakapovaana na Dodoma Jiji FC katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, leo jioni.
Kusimama kwa Ligi Kuu Tanzania Bara ili kupisha maandalizi na ushiriki wa Taifa Stars kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) kumesababisha nyota hao wachelewa kuichezea Simba kwenye ligi, lakini leo huenda wakaanza kuitumikia dhidi ya Dodoma Jiji.

Kiwango bora kilichoonyeshwa na wawili hao katika mashindano ya Simba Super Cup yaliyofanyika wiki iliyopita pamoja na kile cha Lwanga kwenye Kombe la Mapinduzi, kinatoa ishara kuwa nyota hao watakuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachoikabili Dodoma Jiji.
Kwanza ni kwa ajili ya kupunguza pengo la pointi baina yake na vinara wa Ligi, Yanga libakie pointi sita kwani kwa sasa Simba ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 35, wakati Yanga wanaoongoza wana pointi 44.
Kwa vile Simba ina mechi tatu za viporo ili iwe sawa na Yanga kwa idadi ya michezo, ikiwa itapata ushindi leo na pia katika nyingine mbili dhidi ya Azam na Namungo FC, itafikisha jumla ya pointi 44 na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi kwani itabebwa na utofauti wa mabao.
Lakini sababu ya pili ni kujiweka sawa kisaikolojia kwa ajili ya mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo itaanzia ugenini kwa kuikabili AS Vita Club ya DR Congo, Februari 12.
Kama ilivyo kwa Lwanga na Chikwende, ndivyo pia itakuwa kwa Kocha wa Simba, Didier Gomez na yule wa makipa, Milton Nienov ambao nao wamejiunga na Simba hivi karibuni.
Ni mchezo ambao Simba wanapaswa kuwa makini zaidi kwa mbinu ya mashambulizi ya kushtukiza ambayo imekuwa ikitumiwa na Dodoma Jiji, hasa inapokuwa nyumbani katika Uwanja wa Jamhuri, ambako wamekuwa wagumu kufungika.
Katika mechi saba ilizocheza kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, timu hiyo imepata ushindi mara tano na kutoka sare katika michezo miwili.
Simba wanapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji Seif Abdallah Karihe ambaye ndiye amekuwa silaha muhimu ya Dodoma Jiji katika mbinu yao hiyo ya kushambulia kwa kushtukiza na hadi sasa ameifungia mabao matano timu hiyo.
Kocha wa Dodoma Jiji, Mbwana Makatta alisema kuwa vijana wake wako tayari kuikabili Simba. “Ni mechi ya muhimu kwetu ukizingatia hatupo mahali pazuri kwenye msimamo wa ligi hivyo tunahitajika kupata ushindi na wachezaji wangu wanalifahamu hilo.
“Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri lakini sisi tumejipanga vyema na Mungu akipenda tuna imani ya kuibuka na ushindi,” alisema Makatta.
Kwa upande wa Didier Gomez alisema anaingia katika mechi hiyo akiwa na taarifa za kutosha za wapinzani wao.
“Nimewafuatilia kwa ukaribu Dodoma Jiji na nafahamu mengi kuhusu wao.
Lakini pia hata kwa timu nyingine na ligi ya hapa Tanzania kiujumla.
Ni mechi ya ugenini naamini itakuwa ngumu lakini Simba ni timu kubwa na ina uwezo wa kupata ushindi popote kubwa ni wachezaji kujituma na kufanya kile wanachohitajika kufanya,” alisema Gomez.
Mchezo mwingine leo utakuwa ni kwenye Uwanja wa Uhuru Jijini ambapo KMC wataikaribisha Namungo FC.
Katika hatua nyingine, kiungo wa Simba aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu, Jonas Mkude ameungana na kikosi hicho.
Mkude alienguliwa Simba kupisha sakata lake kufanyiwa kazi na Kamati ya Nidhamu ya Simba, kabla ya taarifa kutolewa kwa kupigwa faina na kuruhusiwa kujiunga na wenzake.