Tshishimbi aanzisha jambo huko Msimbazi

UKISIKIA mkwara ndio huu. Siku kama nane tu kabla ya Simba kwenda kuvaana na AS Vita ya DR Congo katika mechi ya kwanza ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kiungo wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa Wakongoman hao, Papy Tshishimbi ametumia salamu ya vitisho Msimbazi akiwaambia watakutana na kipigo kibaya kuliko kile cha msimu wa 2018-2019.
Simba itaanza mechi za Kundi A ugenini kwa kuvaana na AS Vita Februari 12 kabla ya kurudi nyumbani kuwavaa watetezi wa taji hilo, Al Ahly ya Misri, huku wakiwa na kumbukumbu ya kufumuliwa mabao 5-0 kila mechi walipovaana na timu ugenini msimu wa 2018-2019.
Licha ya vipigo hivyo vya ugenini, lakini Simba ilitinga robo fainali nyuma ya Al Ahly baada ya kuwanyoosha AS Vita kwenye mechi ya marudiano na iliyokuwa ya mwisho jijini Dar es Salaam na Tshishimbi alishuhudia akiwa na Yanga na kuionya Simba mapema.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka DR Congo, Tshishimbi alisema Simba lazima ijue a kwamba inakutana na AS Vita tofauti yenye wachezaji wenye kiu ya mafanikio na waliopania mechi hiyo na ile ya marudiano kutokana na kilichotokea 2018-2019.
Tshishimbi alisema maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Simba ni makali wakitamani kushinda vizuri nyumbani kisha kumaliza kazi ugenini.
Kiungo huyo, alisema wanajua kila kitu kuhusu Simba na kwamba ni timu nzuri, lakini hakutakuwa na nafasi ya wapinzani wao kushinda ugenini kwa kuwa ni mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu mpaka na mashabiki wao.
Alisema AS Vita inataka kuanza vizuri katika mechi za kwanza hatua ya makundi na ndio maana maandalizi ni makubwa kujiandaa dhidi ya Simba.
“Tunawajua Simba ni timu nzuri, lakini kushinda hapa Kinshasa halitakuwa jambo ambalo linawezekana kirahisi, hapa tupo katika maandalizi makali sana kuelekea hiyo mechi ya kwanza,” alisema Tshishimbi na kuongeza:
“Tunataka kuanza vyema mechi hizi tutawafunga hapa Simba lakini mpango mzima ni kuwafunga kule Dar es Salaam ili tulipe kisasi ya kututoa mwaka juzi katika hatua ya makundi, hatutaki kufanya makosa mara mbili.”
Katika mechi hiyo ya marudiano ya mwaka juzi, Simba ilishinda 2-1.