Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tukuyu Stars: Waliinusuru Simba kushuka daraja, sasa choka mbaya

Kikosi cha Tukuyu Stars enzi hizo

Muktasari:

Ni jina la timu ya soka kutoka wilayani Rungwe mkoani hapa ambayo iliwashangaza wapenzi wa soka nchini hususan wale wa Simba na Yanga ilipopanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na haikukamatika hadi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

JINA la Tukuyu Sars linapotajwa linawakumbusha mambo mengi wapenda soka nchini.

Ni jina la timu ya soka kutoka wilayani Rungwe mkoani hapa ambayo iliwashangaza wapenzi wa soka nchini hususan wale wa Simba na Yanga ilipopanda Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) na haikukamatika hadi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara.

Tukuyu Stars ilifanya maajabu hayo mwaka 1986 lakini sasa inatapatapa kwenye ligi Daraja la Tatu mkoa, inahaha ili ipande daraja na kuungana na timu za Prisons na Mbeya City za mkoani Mbeya ambazo zinashiriki Ligi Kuu.

Michuano ya Ligi Daraja la Tatu Mkoa ilimalizika hivi karibuni ikishirikisha timu sita, Tukuyu Satrs ilishika nafasi ya tatu na kuiacha Timu ya Wenda ikipanda daraja kuingia la pili.

Katika michuano hiyo Tukuyu Stars ilishinda mechi mbili na kutoka sare mara moja na kufungwa mechi moja.

Juhudi za Tukuyu na mashabiki wa timu hiyo kuhakikisha inapanda hadi Ligi Kuu bado hazijafanikiwa kutokana na matatizo lukuki.

Moja ni ukweli kwamba timu hiyo kwa sasa haina uongozi wa kueleweka. Wachezaji wanajiongoza na kujisimamia wenyewe ili kulinda heshima ya Jina la Tukuyu Stars.

Kocha mchezaji Josiah Steven ambaye pia ndiye kipa wa timu hiyo anakiri kwamba timu yake inakabiliwa na hali ngumu.

“Kwa mfano michuano ya Ligi Daraja la Tatu tumeimaliza kwa wachezaji kujitegemea chakula nyumbani kwao na hata nauli wanatumia za kwao. Muda mwingine tunatembeza bakuli kuomba fedha za mafuta tunapopata gari. Tunacheza mechi bila ya kuwa na maji ya kunywa,’’ anasema kocha huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Crispin Meela anakiri kwamba Tukuyu Stars ya sasa ni kama watoto yatima kwani hawana viongozi.

Anasema uongozi wa serikali ya wilaya umetoa maelekezo kwamba, nguvu mpya zitaingia baada ya timu hiyo kupata uongozi kamili na unaoaminika.

Mmoja wa wachezaji wa timu hiyo, Richard Businge amesema timu yao ingepata msaada wa kifedha ingeweza kupanda daraja mara moja.

Businge ameongeza kudaiwa kwamba wachezaji wengi wanajitolea fedha zao ili kufanikisha ushindi kwa Tukuyu Stars.

“Timu kwa sasa ipo imara na ikipata viongozi inaweza kurudi Ligi Kuu,” alisema.

Wachezaji wanaounda timu hiyo kwa sasa ni Fredy Liyumba, Baraka Mwaipaja, Julius Leonard, Richard Businge, Idd Kakisungu, Agrey Mwakipesile, Ipyana Malakibungu, Joel David, Isack Julius, Emmanuel Cheyo na Yona Mwakatage.

Wengine ni Simoni Ikema, Francis Julius, Musa Mwamulenga, Meshack Juma, Steven Hosiana,

Emiry Bandari, Ibrahim Lubanda, Elia Mwanyingili, Dominick Joakhim, kocha mchezaji, Josiah Steven na Paul Majembe ambaye ni mshauri.

Ilikotoka Tukuyu Stars

Mapema mwaka 1980 katika Mji wa Tukuyu ilianzishwa timu iliyokuwa ikiitwa Limbe. Katika kuipa nguvu timu hiyo mfanyabiashara wa enzi hizo, Lamneck Patel Kaka alijitokeza kuidhamini na kuibadili jina kutoka Limbe hadi kuitwa Tukuyu Stars.

Baadhi ya viongozi wa Tukuyu wanaokumbukwa kwa kuing’arisha timu hiyo ni pamoja na Kaka (muasisi), Mzee Kasyupa (katibu mkuu wa kwanza), Mzee Malakasuka na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya wakati huo, Meja Jenerali Makame Rashid pamoja na Mwakasala.

Kocha wa kwanza alikuwa Athuman Juma wakati nahodha wa kwanza wa timu alikuwa Taisi Mwalyoga.

Lakini baadhi ya makocha waliopita katika vipindi mbalimbali na ambao watakumbukwa kwa michango yao ni Paul West Gwivaha, Robinson Mwaikela, Juma Mwambusi na Chuma Amosi.

Kuvuma kitaifa

Tukuyu Stars ilivuma kitaifa ikiwa na mashabiki wengi baada ya kupanda Ligi Kuu (wakati huo Ligi Daraja la Kwanza) mwaka 1985 na mwaka 1986 ilichukua ubingwa.

Wachezaji wanaoendelea kukumbukwa kwa kuifanya Tukuyu kuwa tishio ni Suleiman Mwankenja, Kelvin Haule, Selemani Mathew, Karabi Mrisho, Yusuf Kamba, Salum Kabunda Ninja (marehemu), Ally Kimwaga, John Alex, Richard Lumumba na Aston Pardon.

Wengine ni Daniel Chundu, Godwin Aswile, Salum Kussi, Asanga Aswile, Mbwana Makata, Peter Mwakibibi, Danford Ngesi, Hussein Zito, Tais Mwalyoga na Simon Mwasakyeni.

Tukuyu inakumbukwa sana mwaka 1987 ambapo iliinusuru Simba kushuka daraja baada ya kukubali kufungana mabao 5-5 katika mchezo wa mwisho wa ligi baina ya timu hizo, mechi ambayo kama Simba ingefungwa basi ingeshuka daraja.

Hata hivyo, baada ya kuiokoa Simba, mwaka 1988 Tukuyu Stars iliteremka daraja lakini katika kujiimarisha mara nyingine timu hiyo iliundwa na vijana wengine wapya.

Miongoni mwa wachezaji waliong’ara kwa nyakati tofauti na Tukuyu Stars ni pamoja na Michael Kidilu, Justin Mtekele, Sekilojo Chambua, Ezekiel King, Shedrack Nsajigwa John Mwansasu, Stephen Mussa, Ivo Mapunda, Jimmy Mored, Seleman Mrisho, Mohamed Kasanda, Mikidadi Maumba, Juma Rajab Mdigo, Peter Luis, John Joseph, Fred Mwailenge na Costa Magoroso.

Miongoni mwa wafadhili waliojitokeza kuimarisha Tukuyu Stars kipindi hicho ni pamoja na Kampuni ya Ghana Building Contractors ikiongozwa na Malakasuka.

Pia, alikuwepo mfanyabiashara aliyejulikana kwa jina la Lampa.

Hata hivyo, mwaka ya 2004 Tukuyu Stars ilipotea katika anga la soka na tangu hapo imekuwa ikihaha katika Ligi Daraja la Nne na inaendelea kuhaha kwa sasa ikiwa Daraja la Tatu.