Trezeguet Farao aliyetamba Afcon, atinga zake Aston Villa

Muktasari:
Aston Villa imeamua kumnunua staa huyu kwa dau la Pauni 8.5 milioni kutoka Klabu ya Kampasa ya Uturuki. Ni hasa huyu Trezeguet?
BIRMINGHAM, ENGLAND.MMOJA kati ya mastaa waliong’ara katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu pale Misri ni staa wa Misri, Mahmoud Hassan maarufu kama Trezeguet.
Aston Villa imeamua kumnunua staa huyu kwa dau la Pauni 8.5 milioni kutoka Klabu ya Kampasa ya Uturuki. Ni hasa huyu Trezeguet?
Apachikwa jina kwa sababu ya David Trezeguet
Jina lake halisi ni Mahmoud Ahmed Ibrahim Hassan maarufu kama Trezeguet na alizaliwa Oktoba Mosi, 1994 katika eneo la Kafr El Sheikh kwao Misri.
Jina la Trezeguet alipewa akiwa na umri wa miaka tisa na kocha wake wa timu ya vijana, Badr Ragab kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuziona nyavu aliokuwa anaulinganisha na ule wa staa wa kimataifa wa zamani wa Ufaransa, David Trezeguet.
Baadaye alijiunga na shule ya soka ya klabu maarufu ya Al Ahly baada ya kukataa uhamisho wa kwenda Qatar. Kisha kwa ushauri wa kocha wake, Ali Maher alibadilisha nafasi yake kurudi kuwa kiungo. Baadaye alipelekwa katika kikosi cha kwanza na Kocha Manuel Jose de Jesus.
Alicheza mechi yake ya kwanza katika pambano la Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya wapinzani wao wa jadi Zamalek, akichukua nafasi ya staa wa Al Ahly, Mohamed Aboutrika huku kocha wake, Jesus akidai alikuwa mmoja kati ya makinda bora aliowahi kukutana nao katika soka.
Alianza mechi yake ya kwanza kwa Al Ahly katika pambano dhidi ya Berekum Chelsea ya Ghana la Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ilikwenda kuchukua michuano hiyo ingawa Trezeguet hakucheza katika pambano la fainali.
Wafaransa, Waingereza wamsaka
Aprili 2013, Trezeguet alipewa ofa ya majaribio katika Klabu ya Nice ya Ufaransa, lakini akaahirihisha majaribio hayo kwa ajili ya kuisaidia Al Ahly ambayo ilikuwa imekumbwa na wachezaji wengi majeruhi katika kikosi chao cha kwanza.
Baadaye alipewa ofa ya majaribio katika Klabu ya Nottingham Forest ya England, lakini klabu hiyo ikagoma kumchukua Trezeguet kwa mkopo baada ya kudai dau la Al Ahly la Pauni milioni moja lilikuwa kubwa kutoka kwa mkurugenzi wa ufundi wa klabu hiyo, Sayed Abdel-Hafiz.
Desemba 2013 alihusishwa kwenda Celtic ya Scotland lakini dili hilo lilikwama baada ya dau lao la Pauni 420,000 kukataliwa. Januari 2015 alitajwa kuwa mchezaji bora wa ndani soka la Misri akiisaidia Al Ahly kutwaa ubingwa wa Misri.
Baadaye klabu hiyo ilidai ingesikiliza ofa za staa huyo kutokana na kukabiliwa na matatizo makubwa ya kifedha. Akaumia bega lake katika pambano dhidi ya Club Africain ya Tunisia na kukaa nje kwa wiki sita.
Atinga Anderlecht, aumia
Licha ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Al Ahly, Wael Gomaa kudai Trezeguet angebakia klabuni hapo, lakini Agosti 6, 2015 alijiunga na Klabu ya Anderlecht ya Ubelgiji kwa mkopo wa Euro 1 milioni. Anderlecht pia ilipewa nafasi ya kumchukua jumla.
Hata hivyo, ujio wake uliharibiwa na majeraha ya bega akiwa na kikosi cha timu ya taifa katika Falme za Kiarabu na hivyo angelazimika kukaa nje kwa miezi kadhaa. Kocha wa Anderlecht, Besnik Hasi alidai ingekuwa vigumu kupima uwezo wa Trezeguet kutokana na tatizo hilo.
Alirudi uwanjani Desemba 2015 na kucheza pambano lake la kwanza la Anderlecht mwezi huo katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Westerlo akiingia uwanjani dakika ya 82 kuchukua nafasi ya Dodi Lukebakio. Kocha wake, Hasi alimmwagia sifa nyingi.Akaanza mechi ya kwanza katika kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Gent, lakini baadaye akaanza kuwekwa benchi huku kocha akidai lugha ilikuwa inamsumbua staa huyo kiasi kwamba alikuwa hafuati maelekezo ya kocha uwanjani.
Mei 2016, Anderlecht ilitangaza kumnasa jumla Trezeguet kwa dau la Euro 2.2 milioni na hivyo kuwa mchezaji wa pili ghali kuuzwa na Al Ahly katika historia baada ya staa wa zamani wa Angola, Flavio Amado.
Apelekwa kwa mkopo Mouscron
Msimu wa 2016-17 chini ya kocha mpya, Rene Weiler alionekana kuanza vyema na kufunga mabao manne katika mechi za maandalizi ya msimu, lakini kununuliwa kwa Nicolae Stanciu kulimfanya apelekwe kwa mkopo Klabu ya Royal Excel Mouscron.
Katika mechi zake za klabu hiyo alihusika na mabao matano akifunga mawili na kupika matano likiwemo la juhudi binafsi dhidi ya Gent ambapo alikimbia akitokea katikati ya uwanja na kufunga.
Kocha wake, Glen De Boeck alidai Trezeguet alikuwa mchezaji mwenye kipaji zaidi klabuni.
Kiwango chake kiliipagawisha klabu yake mama ya Anderlecht huku Kocha Jean-Francois Lenvain akitaka staa huyo arudishwe kikosini. Katika mechi ya mwisho ya msimu, Trezeguet akaifungia Mouscron bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya KV Kortrijk.
Licha ya kufunga mabao saba katika mechi 28, kocha wa Anderlecht alidaiwa kutaka kumuuza Trezeguet kwa madai ya kutokuwa na nidhamu ya mbinu za kimchezo. Mawazo yake yaliungwa mkono na Kocha wa Mouscron, Mircea Rednic.
Galatasaray yamtaka, aenda Kasımpaşa Baada ya kurudi Anderlecht, Trezeguet alihusishwa kwenda Klabu ya Galatasaray ya Uturuki lakini akajikuta akiishia katika Klabu ya Kasımpasa ya hapohapo Uturuki kwa mkopo wa msimu mmoja. Alifunga mabao matano katika mechi zake 12 za kwanza lakini fomu yake ikaharibikiwa na kadi nyekundu aliyopokea katika mechi dhidi ya Bursaspor, akafungiwa mechi tatu.
Aliporudi akafunga bao la tisa dhidi ya Yeni Malatyspor akiwa ni mchezaji wa saba wa Misri kufunga mabao zaidi ya 10 katika Ligi za Ulaya huku pia akipiku rekodi ya Ahmed Hassan kwa kuwa mchezaji wa Misri aliyefunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu ya Uturuki. Kufikia hapo Kasimpasa ilimchukua jumla.
Licha ya kusaini jumla klabuni hapo, Galatasaray ilikutana naye akiwa kambi ya Misri pale Italia.
Inter Milan na Parma pia zilimfukuzia kwa kasi. Klabu ya Slavia Prague ya Czech ilikubali kulipa dau la Euro 5 milioni ambalo Kasimpasa ililitaka na licha ya Trezeguet kupimwa afya na kukubaliana maslahi binafsi na klabu hiyo, lakini baadaye akaamua kubakia Kasimpasa.
Kutokana na kiwango chake cha msimu wa 2017–18 aliteuliwa kugombea tuzo ya mwanasoka bora wa msimu lakini akapoteza kwa staa wa Ufaransa, Bafétimbi Gomis.
Kiwango chake katika ligi na AFCON kimesababisha Aston Villa impeleke katika Ligi Kuu ya England kwa dau la Pauni 8.7 milioni.