TPLB yapangua ratiba Ligi Kuu

BODI ya Ligi Kuu Bara (TPLB) imefanya maboresho ya ratiba yake katika mechi sita ya mzunguko wa tano kwenye Ligi Kuu Bara.

Miongoni mwa marekebisho hayo ni mchezo namba 35 wa KMC dhidi ya Mtibwa Sugar uliopangwa kuchezwa Septemba 27 katika Uwanja wa Uhuru ambapo sasa umebadilishwa na kuchezwa Oktoba 15 katika uwanja huo.

Mchezo namba 33 kati ya Ruvu Shooting na Coastal Union uliopangwa kuchezwa Septemba 26 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Uhuru sasa utachezwa Septemba 29 katika uwanja huo huo.

Mabadiliko mengine ni mchezo namba 34 wa Polisi Tanzania dhidi ya Namungo uliopangwa kuchezwa Septemba 27 saa 8:00 mchana katika Uwanja wa Ushirika Moshi umesogezwa mbele hadi Oktoba 19 saa 10:00 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Mchezo namba 38 kati ya Ihefu na Yanga uliopangwa kuchezwa Septemba 29 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Highland Estate Mbeya kwa sasa utachezwa Novemba 29 katika uwanja huo huo.

Mbali na hayo mchezo mwingine uliofanyiwa maboresho ni ule wa namba 36 kati ya Kagera Sugar dhidi ya Singida Big Stars uliopangwa kuchezwa Septemba 28 saa 8:00 mchana katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa sasa utachezwa Oktoba 21 saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Mchezo namba 37 kati ya Mbeya City na Simba uliopangwa kuchezwa Septemba 28 saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, sasa utapigwa Novemba 23 kwenye Uwanja huo na muda huo huo.

Ratiba ya michezo ya mzunguko wa tano ni Ruvu Shooting dhidi ya Coastal Union Septemba 29, Polisi Tanzania na Namungo Oktoba 19, KMC na Mtibwa Sugar Oktoba 15, Kagera Sugar na Singida BS Oktoba 21, na Mbeya City dhidi ya Simba Novemba 23.

Mingine ni, Ihefu dhidi ya Yanga Novemba 29, Dodoma Jiji na Geita Gold Septemba 27 huku Tanzania Prisons ikiikaribisha Azam Septemba 30.

Sababu iliyotolewa ya maboresho hayo ni kutokana na timu hizo kuwa na wachezaji wao waliojiunga na kikosi cha Stars kinachojiandaa na michezo miwili ya kirafiki ya kalenda ya FIFA dhidi ya Uganda Septemba 24 na Libya Septemba 27.