Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tiote, kama mshumaa katika upepo wa Jangwani

Cheick Tiote wakati wa uhai wake 

Muktasari:

Alianguka mazoezini siku ya Jumatatu na kufa papo hapo baada ya kukumbwa na shinikizo la moyo wakati akifanya mazoezi na klabu yake ya Beijing Entrepreneurs ambayo ilikuwa imemsajili Februari mwaka huu kutoka Newcastle United ya England ambayo aliichezea kwa miaka sita na kutengeneza jina lake.

NI kama mshumaa katika upepo wa Jangwani. Cheick Tiote ametoweka ghafla duniani huku akirudisha nyuma nyakati na kuwakumbusha mashabiki wa soka duniani kifo cha staa wa zamani wa Cameroon, Marc-vivien Foe.

Alianguka mazoezini siku ya Jumatatu na kufa papo hapo baada ya kukumbwa na shinikizo la moyo wakati akifanya mazoezi na klabu yake ya Beijing Entrepreneurs ambayo ilikuwa imemsajili Februari mwaka huu kutoka Newcastle United ya England ambayo aliichezea kwa miaka sita na kutengeneza jina lake.

Huzuni kubwa imewakumba mashabiki wa soka duniani kote wakimkumbuka Tiote ambaye aliwateka kwa soka lake la nguvu ambalo liliendana na soka la Ligi Kuu ya England.

Nyuma yake Tiote ameacha zaidi ya kaka na dada 50 kutokana na kuwa na familia kubwa nchini kwao Ivory Coast. Baba yake alikuwa na mitala na hivyo kuoa wake wanane na Tiote alikuwa mmoja kati ya watoto tisa waliozaliwa kwa baba na mama mmoja.

Katika ukurasa wake wa Facebook kuna picha mbalimbali za staa huyo akiwa na mashabiki pamoja na familia yake. Kocha wa zamani wa England, Steve McClaren ambaye aliwahi kumfundisha Tiote Newcastle aliwahi kuripotiwa akidai kwamba Tiote alikuwa ‘Mtu mwenye tabasamu zuri zaidi la soka’.

Mtu mmoja aliyekuwa karibu na staa huyo alidai kwamba Tiote alikuwa karibu na familia yake ambayo ilikuwa kubwa kutokana na baba yake kuwa na watoto wengi lakini aliwapenda wote kwa amani kubwa bila ya kuwabagua.

“Cheick alikuwa anajivunia sana familia yake na alipenda sana kuwatembelea wakati akiwa nyumbani. Baba yake alikuwa ameoa wake wengi. Cheickh alikuwa wa tisa lakini kulikuwa na kaka na dada wengine 40. Kila wakati alituma pesa nyumbani Ivory Coast. Alikuwa na upendo kwa familia yake,” alisema rafiki huyo.

Kocha wa klabu ya Brighton, Chris Hughton ambayo ndio imepanda Ligi Kuu msimu huu, ndiye ambaye alimsajili Tiote kwenda Newcastle kutoka klabu ya Twente ya Uholanzi kwa dau la Pauni 3.5 milioni mwaka 2010. Anamuelezea Tiote kama kijana mpole.

“Alikuwa mpole sana kwa kila kitu alichofanya. Ilikuwa ni kitu kikubwa kwake kusaini Newcastle. Kocha Steve McClaren aliwahi kumuongelea vizuri kuwa ni mtu ambaye hawezi kukuangusha,” alisema Hughton.

Tiote alizaliwa Juni 21, 1986 katika mji wa Yamoussoukro, Ivory Coast. Alianza kucheza soka la utotoni mitaani kama ilivyo kwa wanasoka wengi wa Kiafrika wanaotamba barani Ulaya. Viatu vyake vya kwanza vya soka alivipata akiwa na umri wa miaka 10.

Alianza kucheza soka la ushindani katika klabu ya FC Bibo ambayo ni ya madaraja ya chini Ivory Coast. Katika mahojiano yake pindi akifika England, Tiote alisema aliacha shule mapema kwa ajili ya kujikita zaidi katika soka.

“Soka siku zote ni kitu kikubwa kwangu na kwa kukulia Abidjan nilijua nilichokuwa nataka kufanya na nilihakikisha kwamba soka linakuwa maisha yangu. Na nilifanya kazi kubwa tena na tena mpaka nikafanikiwa kutimiza ndoto zangu,” Alisema Tiote.

Tiote alienda Ulaya mwaka 2005 baada ya kuonwa na maskauti wa klabu ya Anderlecht ambao waliripoti kipaji chake kwa mabosi wa timu hiyo ambao waliamua kumpa mkataba wa miaka mitatu baada ya kucheza kwa miezi kadhaa katika timu ya wachezaji wa akiba.

Mechi yake ya kwanza ilikuja katika Kombe la Ligi la Ubelgiji dhidi ya Geel ambapo walipoteza kwa Geel na Tiote alikosa penalti yake katika pambano hilo. Mwezi uliofuata alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya dhidi ya Real Betis katika hatua ya makundi ambapo walichapwa 1-0.

Mechi yake ya kwanza ya Ligi ilikuja Machi 18, 2006 akiingia katika kipindi cha pili cha pambano dhidi ya Beveren ambapo Anderlecht ilishinda 4-0. Baadaye alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya Roda FC ya Uholanzi ambapo alicheza msimu mzima na kuonwa na klabu ya Twente.

Ni katika klabu ya Twente ndipo skauti wa Newcastle alipomtupia jicho na kuamuru mabosi wa Newcastle watoe fedha za kumchukua. Katika Ligi Kuu ya England, Tiote aliendana vema na soka la kibabe la ligi hiyo na anakumbukwa zaidi kwa bao lake la kusawazisha dhidi ya Arsenal huku Newcastle ikitoka nyuma kwa mabao manne na kusawazisha yote.

Katika kitu kinachotia huzuni zaidi, mke wa kwanza wa Tiote, Madah alikuwa anatazamia kujifungua mtoto wao wa tatu wiki hii. Tiote pia alioa mke wa pili, Laeticia Doukrou kwao Ivory Coast mwaka 2014 na wakala wake aliweka wazi kwamba ilikuwa ni kitu cha kawaida kwa muumini wa dini ya Kiislamu kuoa wake wawili.