JKT Tanzania V Simba... Patachimbika

Muktasari:
- Simba inayoshika nafasi ya pili na pointi 60, itakuwa wageni wa JKT Tanzania katika mbio za kuwania ubingwa ikiifukuzia Yanga kileleni yenye pointi 70 inayolisaka taji kwa msimu wa nne baada ya kulishikilia kwa misimu mitatu mfululizo tangu ilipowanyang’anya watani zao.
SIMBA inarudi tena uwanjani kuvaana na maafande wa JKT Tanzania. Hicho ni kiporo cha pili kwa Wekundu wa Msimbazi Ligi Kuu Bara baada ya Ijumaa iliyopita kuanza kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa, huku mechi ikiisha kwa matukio kadhaa yenye utata.
Simba inayoshika nafasi ya pili na pointi 60, itakuwa wageni wa JKT Tanzania katika mbio za kuwania ubingwa ikiifukuzia Yanga kileleni yenye pointi 70 inayolisaka taji kwa msimu wa nne baada ya kulishikilia kwa misimu mitatu mfululizo tangu ilipowanyang’anya watani zao.
Mechi hiyo itapigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, uliopo Mbweni jijini Dar es Salaam na Simba ikipania kupata ushindi ili kupunguza pengo la pointi dhidi ya Yanga ambayo imecheza mechi 26 dhidi ya 23 za watani wao hao, huku kukiwa pia na kiporo cha Dabi ya Kariakoo.
Kwa upande wa JKT Tanzania, mechi hii ni fursa ya kuendeleza rekodi nzuri kwenye uwanja wa nyumbani ambao umekuwa mgumu kwa wapinzani kupata ushindi msimu huu.
Mara ya mwisho zilipokutana, Simba ilishinda bao 1-0 lililotokana na penalti ya Charles Jean Ahoua na rekodi zinaonyesha, katika mechi tisa za Ligi Kuu zilipovaana tangu 2018/19, Simba imeshinda mara nane, JKT moja tu bao 1-0 lililofungwa Februari 2020 na Adam Adam.
Mechi ya leo itakuwa ya presha kwa timu zote, licha ya kila moja kuwa na malengo tofauti, Simba ikitaka kuzima kelele za wadau imekuwa ‘ikibebwa’ na waamuzi kwa kutafuta ushindi safi mbele ya maafande hao wanaoshika nafasi ya sita na pointi 32 kupitia mechi 26.
JKT ni timu ya tano iliyoruhusu mabao machache ikifungwa 24, ikiwa nyuma ya Simba (9), Yanga (10), Azam (17) na Singida Black Stars (21), lakini ikiwa ndio timu kinara kwa kutoka sare nyingine (11) hadi sasa, ingawa inaangushwa na safu ya ushambuliaji iliyofunga mabao 24 kama yaliyoruhusiwa na mabeki.
Mechi hiyo ni fursa nyingine kwa nyota wa Simba, Ahoua aliyekosekana mchezo uliopita, Steven Mukwala na Leonel Ateba kuboresha akaunti zao za mabao wakimfukuzia Clement Mzize wa Yanga anayeongoza orodha akiwa na mabao 13.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema “Tunahitaji ushindi. Tunahitaji kuweka presha kwa timu iliyo juu yetu. Hatuwezi kuangalia nyuma, tunahitaji kufunga, kushinda na kusonga mbele. Tunajua JKT wanacheza vizuri sana nyumbani.”
Kwa upande wa JKT Tanzania, Kocha Ahmad Ally alisema wamejifunza kutoka kwa mechi ya duru la kwanza dhidi ya Simba na walilala kwa penalti na safari hii wamejipanga kuzuia makosa ya kizembe na kutumia uwanja wao kama faida.
Akiwa ameshinda michezo miwili ya FA dhidi ya Pamba na Mbeya Kwanza na kutoka sare dhidi ya Namungo na Dodoma Jiji, kocha huyo alisema mechi ya leo itakuwa kipimo halisi cha uwezo wa vijana wa timu hiyo dhidi ya timu kubwa na kuongeza kuwa, lisema morali ya wachezaji wake ipo juu na wanatambua wanacheza dhidi ya moja ya klabu kubwa Afrika.
“Tumekuwa na muda wa kutosha kufanya maandalizi yetu, tunajua kuwa Simba ni timu ya aina gani hivyo naamini mpango wetu utafanya kazi vizuri kikubwa ni watu kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia burudani,” alisema Ally atakayeendelea kuwategemea mabeki Wilson Nangu na Edson Katanga na kipa Suleiman Yakoub kuizuia Simba yenye safu kali ya ushambuliaji chini ya Ahoua, Ateba na Mukwala.