TFF yakwepa mtego wa Ndumbaro

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema hakuna shabiki atakayelazimishwa kuvaa jezi ya Simba wala Yanga ili aruhusiwe kuingia uwanjani wakati timu hizo zitakapocheza mechi zao za nyumbani za hatua ya robo fainali Jumamosi na Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Al Ahly kinyume na kile kilichozungumzwa na waziri wa utamaduni, sanaa na michezo, Damas Ndumbaro.

Ufafanuzi huo umetolewa siku chache baada ya Ndumbaro mwanzoni mwa wiki hii kutangaza kuwa shabiki atakayekwenda uwanjani kutazama mechi hizo anapaswa kuvaa jezi za Simba au Yanga pindi timu hizo zitakapocheza mechi hizo na kinyume na hapo atalazimika kuwa na hati ya kusafiria ya nchi ambayo klabu anayoenda kuishangilia inatokea ila vinginevyo hatoruhusiwa kuingia uwanjani.

 “Ukija uwanja wa Taifa ukiwa umevaa jezi ya Mamelodi Sundowns lazima utuoneshe passport (hati ya kusafiria) ya Afrika Kusini na ukiwa na jezi ya Al Ahly utuoneshe passport ya Misri, nje na hapo ukifanya fujo Polisi watakuchukua ukapumzike kidogo utatoka baada ya mechi,” alinukuliwa Damas Ndumbaro.

Kupitia barua ambayo imeandikwa na katibu wa TFF, Wilfred Kidao kwenda Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), TFF imesema kuwa itahakikisha inasimamia kanuni na taratibu za mpira wa miguu zinafuatwa kikamilifu katika mechi hizo.

"Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linalihakikishia Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuwa mechi husika itachezwa kwa kanuni na taratibu zilizowekwa za soka na namna ya utaratibu wa kuingia uwanjani.

"Kwa hivyo, sio kwamba pasipoti (pasi za kusafiria) zitatumika kama kigezo cha kuingia uwanjani kwa mashabiki wa Mamelodi Sundowns na mtu yeyote kwa sababu mechi ipo kikanuni na taratibu za mpira wa miguu bali sio kwa Idara ya Uhamiaji.

"Timu ya Mamelodi Sundowns imehakikishiwa usalama wao kutoka kwa vyombo husika wakati wote ambao watakuwa nchini na kuheshimu taratibu za mechi yao dhidi ya Young Africans SC, na dhamana hii pia inawahusu maafisa wa mechi, mashabiki wa Sundowns wanaosafiri pamoja na mashabiki wanaoishi Tanzania na anayetaka kuhudhuria mechi hiyo," ilifafanua barua hiyo.                                                                                                     
Mamelodi mambo hadharani

Katika hatua nyingine, Yanga imenasa dondoo tofauti za ujio wa Mamelodi Sundowns, siku ya Machi 28 tayari kwa mchezo dhidi ya timu hiyo ya Afrika Kusini utakaofanyika Machi 30  kuanzia saa 3:00 usiku.

Yanga inafahamu kuwa miamba hiyo ya Afrika Kusini itawasili hapa nchini, Machi 28, siku mbili kabla ya mechi baina yao ikiwa na msafara usiopungua watu 70 na kati yao, 30 ni wachezaji wa timu hiyo.

Katika kundi hilo la watu 40 ambao sio wachezaji, kuna makocha na maofisa wa benchi la ufundi la timu hiyo lakini Mamelodi Sundowns pia itaingia nchini ikiwa na walinzi maalum kwa ajili ya kuwalinda mastaa wa kikosi hicho kwa muda wote ambao watakuwa hapa nchini.

Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya Yanga kimefichua kuwa timu hiyo ya Afrika Kusini itawasili katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kwa ndege ya kukodi ambayo itaisubiria timu hiyo na kuondoka haraka kurejea Afrika Kusini mara baada ya kumalizika kwa mechi baina yao.

"Tunafahamu kwamba ipo hoteli moja iliyo jirani na ufukwe wa bahari ya Hindi ambayo ndio msafara wao utafikia na tayari wameshatuma taarifa za kuomba vibali kwa ajili ya ndege watakayokuja nayo ambayo itakuwa ya kukodi.

"Inaonekana jamaa wamejipanga sana lakini na sisi kwa upande wetu tunaendelea kujiandaa kwa ajili ya mchezo huo kwa vile tukipata ushindi mnono, utatuweka katika nafasi nzuri ya kuingia hatua ya nusu fainali," kilifichua chanzo hicho.

Gazeti hili linafahamu kuwa Mamelodi Sundowns imeamua kuja na walinzi maalum ambao jukumu lao ni kuhakikisha hakuna muingiliano wowote kati yao na wachezaji wa timu hiyo pindi watakapokuwa hoteli au uwanjani wakati wa mechi na mazoezi.

Timu hiyo ya Afrika Kusini pia imepanga kutotumia usafiri wa baso ambao Yanga imeuandaa kwa ajili yao katika kipindi chote itakachokuwepo hapa nchini ambapo itajigharamia na kuandaa usafiri wake na tayari imeshatanguliza maofisa wa awali hapa nchini kwa ajili ya kuweka mambo sawa.