Tembo Warriors kuivaa Haiti robo fainali Kombe la Dunia

KESHO Alhamisi, timu ya Taifa ya watu wenye ulemavu 'Tembo Warriors' itakuwa uwanjani kwenye uwanja wa TFF Riva jijini Instanbul kumenyana na Haiti ikiwa ni mchezo wa hatua ya robo fainali ya mashindano ya kombe la Dunia yanayoendelea nchini Uturuki.

Ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Japan leo jioni  ndio uliwapatia tiketi hiyo huku ushindi huo wakienda kuuapata kwenye dakika 20 za nyiongeza baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 50.

Tanzania imefika hatua hiyo baada ya kumaliza nafasi ya tatu hatua ya makundi wakiwa na jumla ya alama nne kisha wakaitoa Japan katika hatua ya 16 bora ya mashindano hayo

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwa simu na Mwananchi kutoka Uturuki baada ya mchezo kumalizika amesema; "Kwa hatua hii tumekwenda robo fainali. Vijana wamepambana sana," na kuongeza;

"Wanasema tutafika fainali ili kuweka rekodi ya kufika fainali na kuchukua kombe, tuendelee kuwaombea,"

Waziri huyo amesema; "Licha ya baridi huku, vijana wetu wameonyesha uzalendo mkubwa wa kuipigania nchi kwani mchezo ulikuwa mkali sana,"

Haiti ambao ndio wapinzani wao katika hatua hiyo wao waliwatoa Marekani baada ya kuwashushia kipigo cha mabao 6-2