Tatizo Stars ni wachezaji, si kocha
BEKI mahiri wa zamani wa Majimaji na Taifa Stars, Peter Mhina, amesema kuipata timu bora ya taifa, Taifa Stars, itachukua muda kwani wachezaji wa siku hizo walio wengi hawajitambui.
Akizungumza na Mwanaspoti katika mahojiano maalumu mjini Songea, Mhina alisema kuwa inasikitisha kuona kila wakati kikosi cha Stars kinakuwa kibovu na kupata matokeo mabaya wakati wachezaji wapo wengi na wanaishi katika mazingira mazuri, tofauti na miaka ambayo wao walikuwa wakicheza.
Mhina alisema maisha wanayoishi wachezaji wa siku hizi ni ya malipo ya pesa nyingi zinazowafanya wajali zaidi kufanya starehe badala ya kujituma mazoezini na kwenye mechi.
“Natamani kurudi ujanani ili niwaonyeshe mchezaji anatakiwa kuwa na nidhamu gani,” alisema.
“Hata hizo pesa zinazowazuzua kama nikipewa mimi haziwezi kunifanya nishau kazi yangu.
“Hawa wana fursa nzuri hata ya kwenda Ulaya, lakini wanavyofanya ni kama hawataki kwenda huko. Akili zao zimeegemea kwenye starehe na kusahau majukumu yao.
“Ni vigumu sana kupata timu bora ya Taifa maana mfumo wa wachezaji wetu umeharibiwa kuanza kwenye klabu, wachezaji wanalipwa pesa nyingi wanachanganyikiwa, hivyo ni lazima wafanye vibaya.”
Mhina pia alikosoa tabia ya klabu kubadili vikosi kila msimu wa usajili unapofika.
“Hili nalo ni tatizo, hatuna sehemu ya kukimbilia ila kama wachezaji wenyewe wangekuwa wanajitambua tungekuwa na timu bora,” alisema Mhina.
Alisema ukiachana na sababu hiyo pia wachezaji wa siku hizi wanaponzwa na vyakula wanavyotumia.
“Kweli mchezaji unakula chips? Hizo nguvu za kupambana uwanjani utazitoa wapi? Chips zinapaswa kuliwa kama chakula cha nyongeza, ndio maana wakisukumwa kidogo tu wanaanguka,” alisema.