Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania Prisons, Kagera acha tuone itakuwaje!

TZ Pict

Muktasari:

  • Mechi ya mapema leo, itapigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, ambapo wenyeji Tanzania Prisons wenye kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi tatu mfululizo, watakapowakaribisha ‘Wagosi wa Kaya’, Coastal Union wenye morali ya mwenendo mzuri pia.

UHONDO wa Ligi Kuu Bara unaendelea tena leo kwa mechi mbili kupigwa kwenye viwanja tofauti, huku macho na masikio yakiwa ni kutaka kujua timu gani itaungana moja kwa moja na KenGold kushuka daraja na zile zitakazocheza ‘play-off’ ya kubakia.

Mechi ya mapema leo, itapigwa saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, ambapo wenyeji Tanzania Prisons wenye kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi tatu mfululizo, watakapowakaribisha ‘Wagosi wa Kaya’, Coastal Union wenye morali ya mwenendo mzuri pia.

Katika mechi hii, Prisons inayopambania kutoshuka daraja, ushindi tu utaiweka katika nafasi nzuri ya kutoka nafasi ya 14 iliyopo sasa na pointi zake 27 hadi ya 10 au 11, ikitegemea na matokeo ya KMC au maafande wa Mashujaa walioko juu yake.

Kwa upande wa Coastal Union iliyoshinda mechi mbili mfululizo, ina pointi 31 na ushindi utaifanya kusogea kutokea nafasi ya nane hadi ya sita, ikitegemea tu na utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Dodoma Jiji iliyopo juu yake.

Mechi hii itakuwa ni ya kisasi zaidi kwa Prisons ambapo mara ya mwisho zilipokutana kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Coastal Union ilishinda mabao 2-1, Desemba 2, 2024, yaliyofungwa na Hernest Malonga na Maulid Shaaban.

Kocha wa Prisons, Amani Josiah alisema ushindi wa mechi tatu ni motisha kwao ya kupambania timu hiyo isishuke daraja, huku kwa upande wa Joseph Lazaro wa Coastal akilalamikia kitendo cha kukaa muda mrefu bila kucheza mechi za ushindani.

Mechi nyingine ya saa 12:30 jioni, itaikutanisha Kagera Sugar iliyo nafasi ya 15 na pointi 22, ikiwa katika janga kubwa la kupambana kuepuka kushuka daraja, itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba kuikaribisha Mashujaa, iliyo ya 10 na pointi 30.

Kagera ndio yenye presha zaidi kutokana na kutokuwa katika kiwango kizuri, baada ya kuchapwa mechi tatu mfululuzo, jambo linalotishia hali ya kikosi hicho ya kusalia msimu ujao, kwani kama itapoteza itajiweka kwenye mazingira magumu.

Mbali na kiwango kibovu cha Kagera kwa siku za hivi karibuni, moja ya rekodi mbovu kwake ni kutoshinda mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mashujaa, tangu kikosi hicho cha ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’, kipande daraja.

Tangu Mashujaa ipande daraja msimu wa 2022-2023, haijawahi kupoteza mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera, kwani mara tatu zilipokutana, kikosi hicho cha ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’, kimeshinda mara moja na kutoka sare mbili.

Kwa mara ya kwanza timu hizo kukutana, ilikuwa ni Agosti 16, 2023, ambapo Mashujaa ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Adam Adam na Othman Dunia, huku mara ya mwisho zilipokutana zilitoka sare ya 1-1, mechi iliyopigwa Novemba 30, 2024.

Akizungumzia maandalizi ya mechi hiyo, kocha wa Kagera, Juma Kaseja alisema wachezaji wote wako vizuri kiakili na kimwili, huku kwa upande wa Salum Mayanga wa Mashujaa akiwataka nyota wa timu hiyo kuendelea kupambania kikosi hicho.