Taifa Stars kuondoka kesho kwenda Kenya

TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inatarajia kuondoka kesho Machi 13, 2021 kuelekea nchini Kenya tayari kwa michezo miwili ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya nchi hiyo.

Stars imefanya mazoezi ya mwisho leo Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kusafiri kesho Jumamosi mchana kwenda Kenya.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mazoezi hayo, Kocha mkuu wa kikosi hicho Kim Poulsen ameeleza namna safari itakavyokuwa na maandalizi ya timu kwa ujumla kuelekea mechi hizo.

“Tutaondooa kesho mchana kwa ndege na tukifika Nairobi kenya tutaweka kambi tupumzike kidogo kisha tuendelee na mazoezi jioni,"

Tutaondoka na wachezaji wote hawa mliowaona leo (22), pia Himid Mao ambaye amewasili nchini alfajiri ya leo.
Wachezaji wengine wale wa Simba na ambao hawajaripoti kambini watakuja moja kwa moja Kenya kuungana na timu kwaajili ya mechi zitakazofuata,” amesema Kim.

Mechi hizo mbili ni za kirafiki baina ya mataifa hayo mawili na mchezo wa kwanza utakuwa Machi 15 huku ule wa pili ukitarajiwa kupigwa machi 18.

Kwa mujibu wa kocha Kim, yote hayo ni maandalizi kwa ajili ya kujiweka sawa kuelekea mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Guinea ya Ikweta Machi 25 ugenini na ile ya Libya Machi 28 nyumbani kwenye dimba la Benjamin Mkapa.

Wachezaji 22 waliokuwa mazoezini leo ni Juma Kaseja, Metacha Mnata, Kelvin Yondani,  Nicksob Kibabage, Israel Mwenda,  Yassin Mustapha, Dickson Job, Hassan Kessy, Edward Manyama, Salum Abubakar, Ayoub Lyanga, Farid Mussa, Kelvin John, Deus Kaseke, Idd Seleman,  Feisal Salum, Baraka Majogoro, Bakari Mwamnyeto,  Meshack Abraham, Laurent Alfred, Nassor Saadun na Abdul Seleman.