Tabora United, Tanzania Prisons kazi ipo

Muktasari:
- Baada ya kufungwa mabao 3-0 na Simba, Tabora ilijitafuta na kujipata kwa kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Namungo kabla ya kuibalasa Kagera Sugar kwa bao 1-0 mechi iliyopita ikipigwa nyumbani, hivyo kesho itakuwa na kazi ya kutaka kuendeleza wimbi la ushindi mbele ya Prisons ambayo mechi mbili zilizopita ilitoka suluhu dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa.
BAADA ya ushindi wa pili mfululizo katika Ligi Kuu Bara, Tabora United kesho inarudi uwanjani kuikabili Tanzania Prisons inayosaka ushindi wa kwanza, kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.
Baada ya kufungwa mabao 3-0 na Simba, Tabora ilijitafuta na kushinda 2-1 ugenini dhidi ya Namungo kabla ya kuibalasa Kagera Sugar bao 1-0 mechi iliyopita nyumbani, hivyo kesho itakuwa na kazi ya kutaka kuendeleza ubsbe mbele ya Prisons ambayo mechi mbili zilizopita ilitoka suluhu dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa.
Miamba hiyo miwili, ilikutana msimu uliopita kwa mara ya kwanza, huku katika mechi mbili Tabora ilishinda Uwanja wa nyumbani mabao 3-1 kabla ya Prisons kulipa kisasi Jijini Mbeya kwa kuichapa 2-1, hivyo mechi ya leo ni ngumu kutabirika na hasa kutokana na maboresho ya vikosi vyote.
Akizungunza na Mwanaspoti, Kocha wa Prisons Mbwana Makata alisema kitendo cha Tabora kushinda michezo miwili mfululizo inawafanya wao kuchukua tahadhari maana wapinzani wake wameshajenga morali ya ushindi.
“Tunawaheshimu wapinzani wetu Tabora United kwa kuwa wamekuwa na wakati mzuri wa kupata matokeo, lakini hata sisi tumejipanga kupata ushindi wa kwanza ugenini baada ya kucheza michezo miwili ugenini na kutoa sare hivyo kiu yetu ni kushinda dhidi ya Tabora.”
Nahodha msaidizi wa Prisons Salum Kimenya alisema mwaka huu timu hiyo imeanza ligi kitofauti na katika michezo miwili waliyocheza ugenini wamepata sare na huu utakua watatu hivyo wamepanga kupata matokeo mazuri.
Kwa Upande wa Tabora, Francis Kimanzi Raia wa Kenya amesema hakupata muda wa kutosha wa kuiandaa timu baada ya kucheza Jumatano na kutakiwa kucheza tena Jumamosi lakini watapigana kuwa na mwendelezo mzuri.