Stars CHAN matumaini kibao

MARA ya mwisho Tanzania kushiriki michuano ya Chan ilikuwa mwaka 2009 ambapo iliwakilishwa na nyota kibao wakiwa chini ya kocha mwenye hamasa kubwa Mbrazil, Marcio Maximo.

 Nyota 23 wa Stars kwa wakati huo walikuwa Deo Munishi, Salum Swedi, Haruna Moshi, Athuman Idd ‘Chuji’, Kelvin Yondan, Henry Joseph Shindika, Kigi Makasi, Mrisho Ngasa, Geofrey Bonny Namwandu, Jerson Tegete, Mussa Hassan Mgosi, Nurdin Bakari, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Shadrack Nsajigwa, Abdi Kassim ‘Babi’, Nizar Khalfan, Amir Maftah, Shaban Dihile, Shaban Nditi, Farouk Ramadhan Nzee, Juma Jabu Erasto Nyoni na Mwinyi Kazimoto.

Msimu huu unaoanza leo, Taifa Stars iliyopo nchini Cameroon kushiriki michuano hiyo ya Chan kwa mara ya pili inaundwa na jumla ya wachezaji 27 ambao wameeleza matumaini yao juu ya michuano hiyo.

Mwanaspoti ambalo liliweka kambi kwenye kambi ya timu hiyo, kuanzia hotelini hadi mazoezini, leo linakuletea sauti za nyota hao kuelekea Januari 19 watakapoanza kupambania ubingwa huo wa Matafa ya Afrika kwa wanaocheza kwenye ardhi ya nyumbani.


AISHI MANULA (KIPA)

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki michuano hiyo, Manula amesema wako tayari kwa mapambano na wanamuomba Mungu awape afya tele ili wacheze wakiwa fiti zaidi.

“Tuko vizuri kikubwa tunaomba Mungu atupe afya njema ili tuweze kutimiza majukumu yetu. Tunaweza kufanya makubwa zaidi,” alisema Manula ambaye ni kipa wa zamani wa Azam.

JUMA KASEJA (KIPA)

Katika Stars ya sasa Kaseja ndiye mchezaji mkongwe zaidi. Ni nahodha msaidizi wa kikosi hicho na ametoa tathmini yake.

“Natambua ni michuano migumu lakini tutapambana kwa uwezo wetu kuhakikisha tunapata matokeo chanya kwenye kila mechi ili tuzidi kusonga mbele zaidi,” alisema Kaseja ambaye anaichezea KMC.


DANIEL MGORE (KIPA)

Kipa huyu akiwa na klabu yake ya Biashara United huwa anawasha moto kinoma na ikiwa ndio mara yake ya kwanza kuitwa timu ya taifa ameahidi kufanya makubwa zaidi.

“Nyumbani sina cha kurithi zaidi ya jina la ukoo hivyo lazima nipambane ili kuleta furaha kwa ndugu zangu na Watanzania kwa ujumla, naamini hii ni fursa kubwa niliyopata ya kuonyesha kiwango changu na kuongeza thamani yangu pia,” alisema.


SHOMARI KAPOMBE (BEKI)

Moja ya wachezaji mafundi na wenye uwezo mkubwa wa kusakata soka ambao Tanzania inajivunia ni huyu jamaa anayekipga kwenye klabu ya Simba, Kapombe ametoa mtazamo wake na kusema:

“Ni heshima kwa taifa kushiriki michuano hii hivyo tutahakikisha tunarudi nyumbani kwa heshima na hilo litafanikiwa endapo tutajitoa na kufuata yale ambayo tutaelekezwa na bechi letu la ufundi,” alisema Kapombe.


ISRAEL MWENDA (BEKI)

Beki huyu anayeonekana kuwa tunu ya taifa kwa miaka ijayo naye amefunguka mbele ya gazeti hili alivyojipanga kwa Chan 2021.

“Binafsi niko na morali ya kutosha, naamini hii michuano ndio kipimo sahihi cha kiwango chetu kama nchi hivyo kama wachezaji tupo tayari kupambana na kuleta heshima kwa nchi yetu,” alisema Mwenda.


PASCHAL GAUDENCE (BEKI)

Kinda huyu kutoka U-20 ya Azam FC ni moja kati ya wachezaji waliomkosha sana kocha mkuu wa timu hiyo Ettiene Ndayiragije kipindi chote walipokuwa mazoezini. Amesema: “Nashukuru kuwa sehemu ya kikosi cha Taifa chenye wachezaji wengi wakubwa na wenye uwezo mkubwa, naamini kupitia mashindano haya nitaimarika zaidi na kujifunza mengi.”


EDWARD MANYAMA (BEKI)

Akiwa ni nguzo muhimu kwenye klabu ya Namungo, Manyama ameahidi kuwa nguzo pia kwenye timu ya taifa huko Cameroon.

“Niko timamu kiakili na kimwili, naamini naenda kuipambania nchi na kuonyesha thamani ya Watanzania wengi kupitia soka, nitapambana nikishirikiana na wachezaji wenzangu na naamini tutafanya kweli,” alisema.


YASSIN MUSTAPHA (BEKI)

Ni ingizo jipya kwenye timu ya Taifa, lakini Yassin tayari ni nguzo muhimu ya ulinzi katika beki ya kushoto Yanga. Ameahidi kuendeleza mapambano akiwa ndani ya kikosi cha Stars.

“Tunaenda kwenye michuano ambayo ni muda mrefu timu hii ilikuwa haijashiriki hivyo nadhani ni wakati wetu kuipambania na kufanya kila Mtanzania ajivunie kuwepo kwetu kwenye timu hii,” alisema Yassin.


CARLOS PROTAS (BEKI)

Huyu ni kiungo mkabaji asilia lakini baada ya kuonekana anafiti zaidi kucheza kama mlinzi wa kati imeitwa kwenye kikosi cha Stars kwa lengo la kuimarisha ulinzi. Carlos pia amezungumza na Mwanaspoti na kusema: Tumecheza mechi na Congo, kuna vitu zaidi nilijifunza na kuvifanyia kazi na naamini kwenye mechi zijazo nitakuwa bora zaidi.”


BAKARI MWAMNYETO (BEKI)

Akiwa ametoka kuondokewa na mwenza wake pamoja na mtoto, Mwamnyeto amepiga moyo konde na kujitoa kiaskari kwenda nchini Cameroon kulipigania taifa ambapo amesema:

“Mimi ni Mtanzania na ninapohitajika kuitumikia nchi nitafanya hivyo kwenye hali yoyote na sasa kwenye Chan naenda kupambana ili kurudi na heshima kubwa nyumbani.


IBRAHIM AME (BEKI)

Baadhi ya mashabiki wa soka wanamfananisha Ame na beki wa Real Madrid, Raphael Varane kutokana na uchezaji wake. Ame ambaye ni kwa mara ya kwanza kuitumikia timu ya taifa ameeleza matarajio yake. “Ujue mpira ni mchezo wa wazi, nadhani uwezo niliouonesha kwenye klabu niliyopo na nilizopita ndio chanzo cha mimi kuongezwa timu ya taifa, na naahidi kuendelea kujituma zaidi nikiwa kikosini hapa na kuhakikisha haturuhusu mabao,” alisema Ame.


ABDULRAZACK HAMZA (BEKI)

Beki huyu kinda kutoka timu ya vijana ya Mbeya City ameitwa Taifa Stars kwa mara ya kwanza na ameeleza matumaini yake kuelekea Chan.

“Sijawahi kucheza timu yenye wachezaji wengi bora na wakubwa kama hii, hivyo inaonyesha dhahiri kuwa kikosi chetu ni kizuri na kitaenda kufanya makubwa kwenye michuano ya Chan,” alisema Hamza.


SAID NDEMLA (KIUNGO)

Wachezaji wenzake wanamuita ‘Mido’. Kiungo wa Simba, Ndemla anasifika kwa kupiga mashuti na pasi za mbali zenye macho. Naye ametia neno kuhusu michuano hii ya Chan.

“Tuko freshi, kwa maandalizi tuliyofanya yanatosha kufanya jambo kwenye michuano hiyo, uzuri ni kwamba tupo wachezaji wengi na kila mmoja anahitaji kuiwakilisha vyema nchi hivyo kila atakayepata nafasi ya kucheza nadhani atafanya poa,” alisema.


LUCAS KIKOTI (KIUNGO)

Kiungo huyu mnyumbulifu ni moja ya viungo ambao wanajua kuchezesha timu bila ya kuwa na presha yeyote. Kikoti pia Amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka: “Hakuna mchezaji asiyehitaji kushinda mechi na kubeba kombe, wote tunahitaji kufanya hivyo japo tunajua ni ngumu ila tutapambana kwa kushirikiana mpaka mwisho,” alisema Kikoti.

ZUBERI DABI (KIUNGO)

Kutoka Ruvu Shooting mpaka Taifa Stars, Dabi bado anakiwasha ile kinoma noma kwenye dimba la kati. Akizungumza kuelekea michuano ya Chan, Dabi amesema:

“Tunaenda tukijua tutakutana na timu kubwa zaidi, tumejipanga kukabiliana nazo kwa namna yeyote ile uwanjani,” alisema.


FEISAL SALUM (KIUNGO)

Wananchi wa Jangwani wanamuita Fei Toto, kiungo wa mpira kutoka kisiwani Zanzibar, Feisal amesema mengi kuelekea Chan na kubwa zaidi amezungumzia morali ya wachezaji wote.

“Mzee wangu asikwambie mtu, wachezaji wote wana uchu na hii michuano na ndio maana hata mazoezini kila mmoja amejitahidi kuonyesha kile alichonacho kwa kiwango cha juu sana, muda ukifika nadhani tutapambana kiume,” alisema Fei.


KHELFINNIE SALUM (KIUNGO)

Huyu ni kiungo fundi kutoka Zanzibar anayekipiga kwenye kikosi cha vijana cha Azam. Khelfinnie maarufu kama Fini ameiambia Mwanaspoti kuwa anaenda Cameroon kuionyesha dunia nini alichonacho.

“Hii ni nafasi ya kuaminiwa nimepewa, nadhani nilistahili na kwa sasa ndio muda mwafaka wa kuuonyesha ulimwengu mzima nini nilichonacho na kulipambania taifa.”


BARAKA MAJOGORO (KIUNGO)

Kiungo wa mpira kutoka Mtibwa Sugar akiwa anakiwasha dimba la kati huku rasta zake kichwani zikipeperuka, Baraka amesema yuko tayari kwaajili ya michuano na anaamini watafanya vizuri zaidi.

“Binafsi niko vizuri nasikilizia mechi zianze tu, kwa ujumla tumejiandaa vizuri na tunaweza kufanya vizuri zaidi kwenye michuano hii kuliko watu wanavyodhani,” alisema.


SAMUEL JACKSON (KIUNGO)

Bwana mdogo huyu kutoka U-20 ya Ihefu ni moja ya wachezaji wenye nidhamu ya hali ya juu na nguvu za kutosha, ikiwa ni mara ya kwanza kuitwa kwenye timu ya taifa ya wakubwa, amefunguka na kusema: “Namshukuru sana kocha kwa kutambua uwezo wangu na kunijumuisha kwenye timu hii, naahidi kila nikipewa nafasi nitahakikisha nafanya kweli.”


RAJABU ATHUMAN (KIUNGO)

Huyu ni kiungo fundi kutoka kikosi cha Gwambina, Rajabu ni mtaalamu wa kukaba na kupiga masi ndefu zenye macho, akiwa ndani ya timu ya taifa inayowakilisha nchi kwenye mashindano ya Chan amesema: “Haya yanaenda kuwa mashindano yangu ya kwanza makubwa kushiriki, hivyo nitafanya kila liwezekanalo kuhakikisha nakuwa bora kwenye kila mchezo na kuisaidia timu yangu.”


DITRAM NCHIMBI (WINGA)

Spidi na nguvu ndio sifa za huyu jamaa ambaye kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya DR Congo alitoa pasi ya bao la kusawazisha lililofungwa na Danny Lyanga. Nchimbi ameelezea matumaini yake kwenye michuano ya Chan akisema: “Tunaenda kushindana sio kushiriki, uzuri ni kwamba wachezaji wote tuna umoja na ari ya mapambano hivyo naamini tutafanya vizuri,” alisema Nchimbi.


YUSUPH MHILU (WINGA)

Akiwa kwenye kiwango bora kwa miaka ya sasa, Mhilu ni moja ya mawinga wanaotarajiwa kufanya vizuri zaidi kwenye kikosi cha Taifa Stars. Akizungumza na gazeti hili amesema yupo tayari kwa michuano. “Niko fiti, nasubiri michuano ianze tuanze kukimbizana viwanjani, niwatoe hofu Watanzania kuwa jeshi lao tuko vizuri na tunaenda kupambania taifa.”


AYOUB LYANGA (WINGA)

Lyanga ndiye mfungaji wa bao la kusawazisha kwenye mchezo wa majaribio dhidi ya DR Congo uliopigwa mwanzoni mwa wiki hii kwenye dimba la Mkapa na kumalizika kwa sare ya 1-1. Winga huyu hatari amesema “Bao lile ulikuwa mwanzo tu kuelekea Chan, ninaamini kila nikipata nafasi ya kucheza nitafanya vyema na kuisaidia timu yetu kupata ushindi,” alisema Lyanga.


DEUS KASEKE (WINGA)

Mwaisa! Ndivyo wachezaji wenzake kwenye kikosi cha Taifa Stars wanavyomwita katika utani. Kaseke ambaye msimu huu hashikiki akiwa na Yanga, ameahidi makubwa Chan. “Tuko freshi, tumejipanga kucheza na kila mpinzani tutakayekutana naye,” alisema.


FARID MUSSA (WINGA)

Akiwa ni miongoni mwa nyota wa Taifa Stars waliokuwa na kiwango bora kwenye michuano ya Afcon iliyopigwa mwaka 2019 nchini Misri, Farid ameeleza namna alivyojipanga kwa ajili ya Chan. “Niko salama na naendelea na mazoezi na wenzangu ili kutengeneza muunganiko mzuri wa timu, kila mchezaji anatamani kuwa bora kwenye mashindano haya hivyo naamini tunaenda kushindana kweli kweli,” alisema Farid.


JOHN BOCCO (MSHAMBULIAJI)

Huyu ndiye nahodha wa kikosi hicho na kwa nafasi yake amezungumzia mashindano hayo na kusema: “Timu inaendelea vizuri na wachezaji wote wapo tayari kwa mapambano, niwaahidi Watanzania kuwa tunaenda kujitoa kwa nguvu zetu zote kwa heshima ya taifa letu pendwa.”


ADAM ADAM (MSHAMBULIAJI)

Akiwa na bao saba mpaka sasa kwenye Ligi Kuu Bara nyuma ya kinara Bocco mwenye mabao nane, Adam Adam ameeleza namna atakavyokwenda kukiwasha Chan. “Bado sijafunga kwenye mechi nikiwa na Taifa Stars, nadhani huu ndo muda sahihi wa mimi kwenda kuonyesha kuwa sibahatishi.”