Siri chozi la Nabi, asimulia kila kitu

KIKOSI cha Yanga kimerejea nchini jana usiku kilianza safari kutoka Dar usiku kwenda jijini Mbeya, huku kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi akifichua siri ya chozi lake.

Nabi alimwaga chozi mara baada ya kipyenga cha mwisho cha pambano la pili la fainali ya Kombe la Shirikisho, ambapo licha ya Yanga kushinda bao 1-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria, timu hiyo ilishindwa kubeba taji kutokana na faida ya bao la ugenini kuwabeba Waalgeria.

Kocha huyo aliyeandika rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuifikisha Yanga fainali za CAF na pia kupata matokeo ya ushindi ugenini kwenye ardhi ya Waarabu, amefunguka kilichomliza baada ya fainali hiyo, lakini furaha ni kwamba timu hiyo imefikia malengo yaliyoibua pongezi kila kona ya nchi.

Nabi alishindwa kujizuia kulia kama ilivyokuwa kwa straika Fiston Mayele aliyemaliza michuano hiyo akiwa Mfungaji Bora akifunga mabao saba na kuasisti na kocha huyo aliliambia Mwanaspoti sababu ya kumwaga chozi hadharani.

Kocha huyo alisema alijikuta machozi yanamtoka baada ya kuona ndoto yake ya kuwaona Wanayanga na Watanzania wanakosa kuuona ubingwa wa kwanza wa Afrika imeyeyuka na kuongeza aliumia zaidi kuwaona wachezaji wakilia kwa matokeo hayo licha ya kupambana katika muda wote wa dakika 90 zilizokuwa na matukio mengi ya kupunguzwa kasi kutoka kwa wenyeji  USM Alger.

"Kuna wakati niliona ndoto yangu ya kuona Tanzania inapata kombe la kwanza la Afrika inakwenda kutimia, ule muda mchezo ulivyokwisha niliumia kuona hilo, limekwama, ila wachezaji nao walianza kulia waliniumiza sana nikajikuta nami nalia, inaumiza sana," alisema Nabi na kuongeza;

"Mimi sio kocha ninayependa kupoteza malengo, ninaposhindwa kufikia malengo naumia sana hii ndio nidhamu, pia nimekuwa nikiwaambia wachezaji wangu, tunatakiwa kuwa katika nidhamu ya kushinda muda wote, tusikubali matokeo ya kupoteza kirahisi.

"Kila mtu wa Yanga alitamani kuona ubingwa huu unakuja nchini, lakini kuna picha tofauti wako baadhi walioiunga mkono Yanga hata kama sio mashabiki wa timu, niwashukuru sana viongozi wa serikali ya Tanzania kuanzia Rais Samia, ni bahati kuwa na rais kama huyu, niwashukuru pia viongozi wa klabu, mashabiki wetu ambao wakati wote wako na sisi, TFF kwa kila kitu walichofanya kwa ajili ya Yanga.

Aidha Nabi alifichua kuwa waliushika vizuri mchezo huo baada ya kuwasoma vizur USM Alger na kubadilisha kila kitu kuhusu mbinu hatua ambayo iliwapa ugumu kucheza kwa ubora wao.

Alisema anajivunia wachezaji wake kwa jinsi walivyocheza kwa nidhamu kubwa muda wote wa mchezo huo na kuwapa ugumu USM Alger kufanya lolote hatari ingawa ushindi wao haukutosha.

"Tuliwasoma vizuri jinsi wanavyocheza (USM Alger) lakini pia tulijua wanachezaji nyumbani tukasema tutumie mfumo tofauti ambao hatyjawahi kuutumia hapa Yanga ambao ulitusaidia sana, niwapongeze wasaidizi wangu wote kazi nzuri imetupa heshima lakini pia wachezaji kila mmoja anafurahia jinsi Yanga ilivocheza, nimeongea na makocha mbalimbali na hata wachezaji wa wapinzani nao wamesifu jinsi wacherzaji walivyojituma