Singida yaaga Kombe la Shirikisho Afrika

WAWAKILISHI pekee waliokuwa wamebakia kwenye Kombe la Shirikisho Barani Afrika, Singida Big Stars imetupwa nje rasmi katika mashindano hayo baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-1 dhidi ya Future FC kutoka nchini Misri.
Katika mchezo huo wa marudiano uliopigwa Uwanja wa Al-Salaam jijini Cairo, Singida ilikuwa ikihitaji ushindi au sare ya aina yoyote ili kutinga hatua ya makundi baada ya mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam kushinda 1-0.
Future ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya nne tu ya mchezo kupitia kwa Ahmed Atef huku Singida ikijibu mapigo hayo baada ya kusawazisha dakika ya 28 kupitia kwa nyota wa timu hiyo raia wa Togo, Marouf Tchakei.
Wenyeji walipata bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika ya 52 kupitia kwa Ahmed Refaat kufuatia nyota wa timu hiyo, Ahmed Atef kudondoshwa eneo la hatari na kipa, Beno Kakolanya wakati, Omar Kamal akifunga la tatu dakika ya 68.
Wakati Singida ikiendelea kulisakama lango la wapinzani, ilijikuta ikipachikwa bao la nne dakika za mwishoni mwa mchezo kupitia kwa kiungo, Nasser Maher hivyo kutolewa rasmi kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 4-2.
Katika mchezo huo Singida itajilaumu yenyewe na hii ni kutokana na wenyeji kucheza pungufu baada ya nyota wa Future, Mahmoud Rezq kuonyeshwa kadi nyekundu dakika 55 kufuatia kumchezea madhambi kiungo, Morice Chukwu.
Singida ilifika hatua hiyo baada ya kuiondosha klabu ya JKU ya visiwani Zanzibar katika mchezo wa awali wa michuano hii kwa jumla ya mabao 4-3 wakati huo ikiwa na aliyekuwa Kocha Mkuu Mholanzi, Hans Van Der Pluijm.
Modern Future: Mahmoud Genish - Omar kamal, Basem Ali, Khaled Reda, Mahmoud Rezq - Ghanam Mohamed, Babatunde Bello (Aly Elfeel 71), Aly Zazaa (Nasser Maher 35), Abdelkabir El Ouadi ( Moahmed Farouk 85), Ahmed Refaat (Mohamed Nossier 85) - Ahmed Atef (Marawan Mohsen 85)
Singida Big Stars: Beno David Kakolanya - Kelvin Kijili, Biemes Carno, Hamadi Tajiri, Gadiel Michael Kamagi - Nicholas Gyan, Yusuph Kagoma, Morice Chukwu, Duke Abuya - Marouf Tchakei, Elvis Rupia