Singida waleftishwa fasta WhatsApp

UONGOZI wa timu mpya kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao, Singida Big Stars (zamani DTB) ‘umewaleftisha’ mastaa wake kibao walioipandisha daraja timu hiyo na kuanza kusuka upya chama hilo.

Mwanaspoti limejiridhisha kuwa, Singida imeachana na robo tatu ya wachezaji wake waliokuwepo msimu huu na kubakiza wasiozidi 10 na sasa imeanza kusajili wengine wapya.

Taarifa za kuaminika tayari nyota hao wakiongozwa na Yanick Bazora, Yusuph Mlipili, David Mwantika, Majaliwa Shaban na Tafdazwa Kutinyu, Majaliwa Shaban James Msuva na wengine wengi wamepewa barua za kuachana na timu hiyo sambamba na kuleftishwa kwenye magrupu yote ya ‘Whatsapp’ ya timu hiyo.

Moja ya wachezaji kati ya hao walioleftishwa ambaye hakuwa tayari jina lake kuwekwa wazi, ameliambia Mwanaspoti kuwa uamuzi huo umekuwa ghafla lakini hawana budi kukubali.

“Ndivyo maisha ya soka yalivyo, ghafla tu tumetolewa kwenye magrupu ya timu na kuagwa hivyo hatutokuwa ndani ya timu ile msimu ujao,” alisema nyota huyo na kuongeza;

“Wakati timu inapanda tuliambiwa tutakaa mezani kuzungumza mikataba mipya kwaajili ya msimu mpya Ligi Kuu, lakini wakati tunasikilizia kuitwa ndio imetokea hivyo tumeachwa.”

Mtendaji mkuu wa timu hiyo, Muhibu Kanu alieleza timu hiyo kila jambo inalofanya imezingatia matakwa ya viongozi wa timu na kuhusu wachezaji ni kulingana na ripoti ya benchi la ufundi.

“Kila kitu tunakifanya kwa ubora, kwa wachezaji watabaki wale waliopendekezwa na benchi la ufundi na wengine tutaachana nao kwa wema pia tutasajili wengine ili kuwa na timu yenye ushindani kwenye ligi,” alisema Kanu.