Singida United yatinga fainali kibabe

Muktasari:
Singida United, Mtibwa Sugar zinakutana kwa mara ya kwanza katika fainali ya Kombe la FA
Dar es Salaam. Singida United imetinga fainali ya Kombe la FA baada ya kuichapa JKT Tanzania kwa mabao 2-1 baada ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Nafua, Singida.
Singida United sasa itavaana na Mtibwa Sugar katika fainali ya FA itakayopigwa Juni 2 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Ikicheza mbele ya mashabiki wake Singida United ilikubali kuruhusu bao la mapema lililofungwa na Hassan Matelema wa JKT Tanzania kabla ya wenyeji hao kubadilika kipindi cha pili na kusawazisha Tafadzwa Kutinyu.
Shujaa wa Singida United alikuwa Mzimbabwe Kutinyu aliyefunga mabao yote dakika ya 53 na 97 na kuivusha kwa mara ya kwanza timu hiyo kucheza fainali ya Kombe la FA ambalo mshindi wake atajinyakulia Sh50milioni.
Mashabiki wa Singida United waliongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba walishangilia kwa ishara ya kupaa baada ya Kutinyu kusawazisha bao na kuongeza jingine.
Katika mchezo huo, JKT Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 38 kupitia Matelema lakini Singida walisawazisha na timu hizo kumaliza dakika 90 kwa sare ya bao 1-1 huku mwamuzi Hans Mabena akikataa bao la Singida dakika ya 65.
Uamuzi wa kuongeza dakika 30 ulionekana kupingwa na kocha wa JKT Tanzania, Bakari Shime aliyekuwa amefanya mabadiliko ya kipa dakika ya 90 akiamini wanakwenda kwenye matuta, lakini mambo yakawa tofauti.