Singida Black Stars ina saa 48 tu

Muktasari:
- Singida imesaliwa na mechi mbili za kufungia msimu ikiwamo ile ya Tanzania Prisons, huku ikiwa imekata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao kwa kujihakikisha kumaliza nafasi ya nne mbali na kutinga fainali ya FA dhidi ya Yanga.
KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amesema amebakiza siku mbili ikiwa sawa na saa 48 za maandalizi ya mwisho kabla ya kuifuata Dodoma katika pambano la Ligi Kuu Bara, huku akifurahia kufikia malengo ya kuipeleka timu hiyo katika michuano ya kimataifa.
Singida imesaliwa na mechi mbili za kufungia msimu ikiwamo ile ya Tanzania Prisons, huku ikiwa imekata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao kwa kujihakikisha kumaliza nafasi ya nne mbali na kutinga fainali ya FA dhidi ya Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema anafurahia mafanikio kwa kuwa amefikia malengo yaliyokuwa yanakusuduiwa na wana Singida kucheza michuano ya kimataifa.
“Nina siku mbili za kukamilisha programu ya mazoezi kabla ya kikosi hakijaanza safari Juni 16 kuifuata Dodoma Jiji mchezo ambao ni muhimu kupata matokeo ili tujitengenezee mazingira mazuri kwenye msimamo licha ya kukata tiketi ya kimataifa,” alisema Ouma.
“Hautakuwa mchezo rahisi lakini tuna uhakika wa kufanya vizuri kutokana na ubora wa kikosi lakini pia wachezaji wapo kwenye morali nzuri ya kuweka rekodi nzuri msimu huu ambao haukuwa rahisi mipango sahihi ndio imetufanya tufike hapa tulipo sasa.”
Akizungumzia maandalizi alisema yanakwenda vizuri na wachezaji wapo tayari kupambania nembo ya timu yao kilichobaki ni kufanya kwa vitendo kiwanjani wakitumika kwa dakika 90.
“Tunaiheshimu Dodoma Jiji ni timu shindani hatutarajii mteremko, lakini tunaamini dakika 90 ndizo zitakazoamua ubora wa mshindi, Jumatatu tunaanza safari kuelekea Dodoma tayari kwa mchezo wa ligi na tutarejea kumalizana na Tanzania Prisons.”
Ouma alisema licha ya kufikia malengo wanasaka rekodi kwa kumaliza msimu katika kilele cha ubora akiutaja mchezo wa fainali FA dhidi ya Yanga utakaopigwa Juni 28 kuwa na umuhimu mkubwa.