Fadlu atoa siku mbili Simba

Muktasari:
- TPLB imeahirisha mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara duru la pili kutoka Jumapili Juni 15 hadi Jumatano Juni 25 mwaka huu ambapo itachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.
SIKU moja baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutangaza kusogezwa mbele kwa mchezo wa Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba, kocha wa Simba, Fadlu Davids ametoa mapumziko ya siku mbili kwa wachezaji wa timu hiyo.
TPLB imeahirisha mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara duru la pili kutoka Jumapili Juni 15 hadi Jumatano Juni 25 mwaka huu ambapo itachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.
Awali mchezo huo ulipangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu, lakini uliahirishwa baada ya Simba kudai kunyimwa haki yao ya kikanuni ya kufanya mazoezi uwanja wa mechi siku moja kabla, ndipo TPLB ikapanga ufanyike Juni 15, kabla ya Yanga kugomea ratiba hiyo na sasa imeamuliwa kuchezwa Juni 25.
Fadlu amesema walikuwa na program kwa zaidi ya wiki wakijiandaa na mchezo huo dhidi ya Yanga uliotarajiwa kuchezwa kesho Jumapili, lakini kutokana na mabadiliko ya ratiba wameamua kutoa mapumziko kabla ya kuvaana na KenGold.
“Ni kweli tumetoa mapumziko ya siku mbili kwa wachezaji kuanzia leo Jumamosi na kesho Jumapili, Jumatatu timu itatakiwa kurejea haraka kambini tayari kwa maandalizi ya kuikabili KenGold,” amesema Fadlu.
Wakati huohuo, Daktari wa Simba, Edwin Kagabo, amezungumzia hali ya wachezaji waliokuwa majeruhi akiweka wazi kuwa wote wanaendelea vizuri na wameanza mazoezi.
“Hatuna majeruhi, wachezaji wote wamerudi kwenye uwanja wa mazoezi, kilichobaki kocha kuamua nani amtumie kwa mchezo ulio mbele yetu.
“Moussa Camara, Mzamiru Yassin na Valentino Nouma wote wamerejea kwenye hali zao za utimamu na wameshaanza mazoezi, hivyo hatuna majeruhi hata mmoja,” amesema dokta huyo.
Simba imebakiza michezo mitatu ya ligi msimu huu ambapo Juni 18 itakuwa ugenini kukabiliana na KenGold, kisha Juni 22 itaikaribisha Kagera Sugar, kabla ya Juni 25 kumaliza msimu kwa kucheza dhidi ya Yanga.