Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bosi TFF atia neno ishu ya Mnguto

BOSI Pict

Muktasari:

  • Taarifa hiyo ilikuwa kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto aliyeandika barua ya uamuzi huo.

TAARIFA iliyoshtua jana  haikuwa kupangwa upya kwa tarehe ya kiporo cha Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba, bali ile iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) yenye mistari minne tu, lakini ikatingisha huku bosi wa zamani wa kamati ya sheria TFF akisema suala hilo limechelewa kuchukuliwa uamuzi.

Taarifa hiyo ilikuwa kujiuzulu kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB), Steven Mnguto aliyeandika barua ya uamuzi huo.

Ndani ya taarifa hiyo kukawa na uamuzi wa kumsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo uliofanywa na Rais wa TFF, Wallace Karia.

Hali hiyo inaifanya TPLB kusalia na kiongozi mmoja wa juu, Makamu Mwenyekiti, Nassoro Idrissa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Azam FC.

Mnguto ambaye alikuwa amebakiza miezi michache kumaliza muda wake baada ya kupoteza sifa kufuatia Coastal Union iliyompa nafasi hiyo kupata viongozi wapya, amejiuzulu TPLB ikiwa inakabiliana na utata wa mchezo namba 184 wa dabi.

Taarifa kutoka ndani ya TFF ni kwamba, chekeche hilo la viongozi linaweza kuwa endelevu kwa vigogo wengine kuondoka ndani ya mamlaka hizo mbili.


MSIKIE MVELA

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria wa TFF wa zamani, Eliud Mvela akizungumzia hatua ya kujiuzulu kwa Mnguto na kusimamishwa Kasongo, alisema hatua hiyo imechelewa kwani ilipaswa kuchukuliwa muda mrefu.

Mvela alisema uamuzi huo utarudisha utulivu kwenye mchezo huo ambapo pia utakuwa ni msaada mkubwa kwa viongozi wanaosalia kurudi kutumia kanuni badala ya busara.

“Kwanza niseme hizi ni hatua ambazo zimechelewa sana, ukitazama kwa picha kubwa kwa mtazamo wangu utaona kuna nguvu ya usimamizi wa serikali,” alisema Mvela na kuongeza:

“Huwa nasikia watu wanasema serikali haitakiwi kuingilia michezo, ni kweli lakini serikali ina nafasi yake ndani ya TFF hata katiba yetu inaeleza kutakuwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ambalo ndio serikali.

“Serikali haiwezi kutulia tu kuogopa kushauri mambo endapo inaona kwamba kuna jambo zito linaendelea linaloweza kuleta shida kubwa. Tukumbuke kuna kuandaa mashindano makubwa ya Afcon na Chan ndio serikali hii hii inatumia gharama zake kuwezesha hayo yote.

“Mnguto alichelewa kuchukua uamuzi kwa kuwa mambo yalianza kuharibikia kwenye kamati ambayo anaiongoza. Alipaswa kujitathimini muda mrefu lakini pia rais wa TFF amefanya jambo zuri kumwajibisha mtendaji wa Bodi, hilo lipo kwenye mamlaka yake kwani huyu anapatikana kwa kuomba na sio kuchaguliwa hasa mambo kama yanaonekana kwenda vibaya kama ilivyo.

“Hili lililofanyika TFF inapaswa kulibeba kwa mrengo chanya kwa kuwa linakwenda kuwasaidia kurudisha utulivu lakini pia  wanatakiwa kubadilika kuanza kutumia kanuni na si busara tena.

“Utaona hili suala liliharibikia kwenye ile Kamati ya Usimamizi wa Ligi, niseme tu uongozi wa Bodi, bado upo kamili kwa kuwa kuna Makamu Mwenyekiti amebaki, lakini ilipaswa nayo ivunjwe na zingine zifanyiwe tathimini hazifanyi uamuzi wa haki.

“Zipo kamati zinafungia watu vibaya, mtu kafanya kosa dogo anafungiwa maisha unajiuliza kwa nini apewe adhabu kubwa kama amepanga matokeo au ametumia rushwa.”

Naye Rahim Kangezi ambaye ni mmiliki wa klabu ya African Lyon, aliunga mkono hatua hizo zilizochukuliwa huku akiipongeza Yanga kwa kufanya uamuzi mgumu utakaozisaidia timu zingine mbele ya safari.

“Kwangu nimepokea kwa furaha uamuzi huu, kwanza niwapongeze Yanga kwa kujitoa muhanga kutaka mabadiliko, unajua sisi tulipokuwa tunalalamika huko nyuma tulionekana wakorofi na kwa kuwa tulikuwa klabu ndogo tukazimwa kirahisi,” alisema Kangezi.