Mnguto ajiuzulu, Karia amsimamisha Kasongo TPLB

Muktasari:
- Taarifa iliyotoka usiku huu kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema Mnguto ameandika barua ya kuachia nafasi hiyo.
Saa chache baada ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kupanga tarehe ya mchezo wa Yanga dhidi ya Simba, Mwenyekiti wake Steven Mnguto amejiuzulu.
Taarifa iliyotoka usiku huu kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imesema Mnguto ameandika barua ya kuachia nafasi hiyo.
Hatua hiyo imekuja wakati ambao Mnguto amebakiza miezi michache kuachia nafasi hiyo baada ya Coastal Union kupata uongozi mpya.
Hata hivyo, sababu ya mwenyekiti huyo kujiuzulu wadhifa huo haikuelezwa.
Wakati Mnguto alijiuzulu, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amemsimamisha kazi Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPLB, Almas Kasongo. Hata haijaelezwa sababu ya kusimamishwa kwake.
Uamuzi wa Karia kumsimamisha Kasongo unakuja siku chache tangu Yanga imuorodheshe kwenye kundi la watu iliokuwa inashinikiza wajiuzulu kufuatia sakata la Dabi la Kariakoo ambayo iliahirishwa na TPLB Machi 8, mwaka huu katika mazingira ambayo yalilalamikiwa na wenyeji wa mchezo, Yanga kuwa hayakuzingatia kanuni za uendesha Ligi Kuu.
Uamuzi huo unaifanya TPLB kwa sasa kuwa chini ya Makamu Mwenyekiti, Nassoro Idrissa.