Singida Big Stars bado Uwanja wa Liti tu

MECHI tisa za Singida Big Stars zimeipa alama 12 na kukalia nafasi ya saba ikilingana kila kitu na Kagera Sugar, huku timu hiyo ikiwa imepata alama tisa kati ya hizo 12 kwenye viwanja vitatu tofauti vya ugenini.

Timu hiyo yenye mastaa 12 wa kigeni, imeshindwa kuibuka na ushindi wowote kwenye uwanja wake wa nyumbani (Liti) uliopo Mjini Singida.

Katika mechi zote nne ilizocheza kwenye uwanja huo, Singida imeambulia kichapo kimoja cha mabao 2-1 dhidi ya Simba, huku mechi zote tatu zilizobaki, ikitoa suluhu tasa dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons, sare ya mabao 2-2 na Ihefu FC.

Hii inaifanya timu hiyo kutokuwa na matumizi bora ya uwanja wake wa nyumbani, kwani katika mechi hizo zote kama ingepata ushindi, ingekuwa nafasi za juu kwenye msimamo, tofauti na nafasi ya saba iliyopo ambayo inadhihirisha ina kazi kubwa ya kufanya.

Hali ni tofauti na mechi tano ilizocheza ugenini hadi sasa, imefanikiwa kushinda tatu dhidi ya Mtibwa Sugar (Manungu), Namungo (Majaliwa) na Mashujaa (Lake Tanganyika), huku ikipoteza mechi kubwa mbili dhidi ya Yanga na Azam zote zilichezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.