Thadeo Lwanga azifuata Simba, Yanga CAF

Muktasari:
- Lwanga ambaye aliichezea Simba kwa misimu miwili kati ya mwaka 2020 hadi 2022, hili linakuwa ni taji lake la pili la Ligi Kuu akiwa na wababe hawa wa Rwanda tangu ajiunge nao mwaka 2023 akitokea AS Arta Solar ya Djibouti.
KIUNGO wa zamani wa Simba, Thadeo Lwanga, 31, amebeba ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda akiwa na APR, leo Jumamosi baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rwamagana City na kufikisha pointi 64.
Lwanga ambaye aliichezea Simba kwa misimu miwili kati ya mwaka 2020 hadi 2022, hili linakuwa ni taji lake la pili la Ligi Kuu akiwa na wababe hawa wa Rwanda tangu ajiunge nao mwaka 2023 akitokea AS Arta Solar ya Djibouti.
Hili linakuwa ni taji la 23 kwa APR, lakini ni ubingwa wao wa sita mfululizo tangu msimu wa 2019/20.
Hiyo inamaanisha kuwa wamefuzu Ligi ya Mabingwa Kwa msimu ujao kama ilivyo Kwa Simba na Yanga za Tanzania.
Vilevile kwa msimu huu, hili linakuwa ni taji lapili kuchukua kwani ilishachukua taji la Rwandan Cup ambapo iliichapa Rayon Sports kwa mabao 2-0 katika fainali.
Mbali ya mabingwa, APR, wapinzani wao wa karibu Rayon Sports wao wamejihakikishia nafasi yapili katika msimamo ambayo itawawezesha kushiriki michuano ya Shirikisho Afrika.
Ligi ya Rwanda ambayo ina timu 16, hadi sasa imefikia raundi ya 29 na itamalizika wikiendi ijayo ambapo timu zote zitashuka dimbani kucheza mechi za mwisho.