Prime
Simba yaweka jina la Samia kwenye jezi

Muktasari:
- Jezi ya sita ya Simba, ambayo pia itazinduliwa saa 1 usiku, itakuwa maalumu kwa Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji, ambaye amefanya usajili mkubwa kwa msimu ujao wa 2023/24.
Uongozi wa Simba, umetaja majina sita ya viongozi wa Serikali, ambayo yataandikwa nyuma ya jezi zitakazozinduliwa leo, huku la kwanza likiwa la Rais Samia Suluhu Hassan.
Simba, ambayo leo inazindua jezi yake ya msimu wa 2023/24 imepeleka kileleni aina sita za jezi, na ya pili ni maalumu kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Hussein Mwinyi, ya tatu ni kwa Makamu wa Rais, Philip Mipango, ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na ya Spika wa Bunge, Tulia Akson.
Jezi ya sita ya Simba, ambayo pia itazinduliwa saa 1 usiku, itakuwa maalumu kwa Rais wa Heshima wa Simba, Mohammed Dewji, ambaye amefanya usajili mkubwa kwa msimu ujao wa 2023/24.
Akizungumza kabla ya kuanza safari ya kupanda mlima Kilimanjaro, Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula alisema wameamua ‘ku-dedicate’ jezi hizo kutokana na umuhimu wa watu hao katika maendeleo ya nchi.
Kajula alisema wanapoanza 'Wiki ya Simba' kutakuwa na mnada wa kuuza jezi hizo mpya na fedha zitakazopatikana zitakwenda wodi ya mama na mtoto katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
"Hakuna asiyejua umuhimu wa mama, tutakwenda kujenga wodi ya mama na mtoto, ambayo naamini itakuwa msaada mkubwa kwa kuokoa maisha ya mama na mtoto katika hospitali hiyo,” alisema Kajula.
Mgeni rasmi katika halfa ya kuwaaga watu maalumu ambao wamepeleka jezi hizo kileleni, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya aliyemuwakilisha Mkuu wa MKoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema ni historia katika mlima huo mkubwa Afrika.
Mwaipaya alisema kwa mara ya kwanza tukio la kupandisha mlima kumekuwepo na zoezi la kuzinduliwa jezi na mwanzo timu zilikuwa zinapeleka tu bendera zao.
"Simba wana bahati kubwa ya kuwa wa kwanza kufanya tukio hili, ambalo ni la kwanza duniani na pia ilikuwa timu ya kwanza kupeleka bendera yake katika kilele cha mlima Kilimanjaro 2019," alisema.
Meneja wa Habari na Mawasiliano ya Simba, Ahmed Ally alisema sababu kubwa ya kwenda kuzindua jezi kileleni ni kutokana na kuamua kuisapoti serikali.
“Tumekua tukitumia jezi yanye maandishi ya 'Visit Tanzania' kuitangaza nchi yetu, lakini sasa tumeamua kufika kileleni kuhakikisha utalii wa ndani unazidi kukua," alisema Ally.