Simba yataja mambo matatu fainali kupigwa Zanzibar

Muktasari:
- Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa sababu ya wao kupambana kucheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni kuwafikiria zaidi mashabiki wao.
Simba imetamba kuwa haina hofu yoyote kucheza mechi katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ikiwa ni siku moja baada ya kuwatangazia mashabiki wake kuwa mechi yake ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itachezwa hapo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa sababu ya wao kupambana kucheza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa ilikuwa ni kuwafikiria zaidi mashabiki wao.
“Sasa nguvu yetu yote inaelekea Uwanja wa Amaan. Wapo wanaofikiri kwamba Simba inaongopa kucheza Amaan. Lakini sababu ya msingi ni kutokana na ukweli kwamba hili ni tukio kubwa la kihistoria kwa klabu ya Simba.
“Na tulitegemea watu wengi waje katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuja kuona tukio hilo kubwa. Watu wengi walikuwa na shauku ya kuja kuona huo mchezo. Lakini sababu nyingine ambayo hatukata mechi kuchezwa zanzibar ni kwamba gharama inakuwa kubwa mno kwa mashabiki wetu.
Kwa Dar es Salaam mechi ikiisha hata saa 2 saa 3 usiku mnaweza kupanda Coaster zenu mkarudi nyumbani lakini kwa Zanzibar lazima mlale,” amesema Ally.
Ahmed Ally amesema kuwa shabaha yao ni kutwaa ubingwa na wana imani ya kufanikisha hilo ndani ya Uwanja wa New Amaan Complex.
“Baada ya mechi kupelekwa Amaan sisi kama timu kubwa tunapaswa kufanya maandalizi ya kuelekea Amaan. Tunaanza maandalizi kwa sababu lengo letu linabaki kuwa lilelile nalo ni kutwaa ubingwa. Sasa hivi ni harakati za kupigania ubingwa.
“Uwanja wa Amaan ndio ambao unetupeleka fainali ya Kombe la Shirikisho baada ya miaka mingi kupita na Uwanja huuhuu ndio utatupa ubingwa wa Afrika. Simba hii haishindwi kupata matokeo mazuri Amaan, Zanzibar.
“Bao mbili ambazo ametangulia RS Berkane kwetu ziwe kama chachu ya kutuongezea nguvu. Kila ambaye alitufunga nyumbani kwake, nyumbani kwetu tulimfunga. RS Berkane alitufunga nyumbani kwake na sisi kwetu tutamfunga.
“Itakuwa ni fedheha isiyo na kifani kombe lipo nyumbani kwetu halafu kombe liondoke. Hii itakuwa ni jambo la kutuumiza. Tuna kila sababu, tuna kila nguvu na tuna kila uwezo wa kulibakisha kombe nyumbani,” amesema Ahmed Ally.
Ally amesisitiza kuwa kila shabiki wa Simba atakayekwenda kutazama mechi hiyo, aende akiwa amevaa jezi nyekundu.
Kuhusu tikiti zilizokuwa zimeuzwa
Awali kabla ya kuelezwa kuwa mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Amaan, tayari Simba ilishaanza utaratibu wa kuuza tiketi ambapo Ahmed amesema waliokuwa wamenunua tiketi wazitunze kwani watazitumia kwenye Tamasha la Simba Day.
"Kwa wale ambao walishanunua tiketi zao, waendelee kuzitunza kwani zitatumika kwenye Tamasha la Simba Day, mchezo wa Zanzibar unawekewa utaratibu mpya." alisema Ahmed.