Kiduku afichua ukimya wake, atamba kurejea ulingoni kivingine

Muktasari:
- Kiduku ambaye ni bondia kutoka mkoani Morogoro mwenye rekodi ya mapambano 35, akishinda 24 (9 KO), kupigwa 10 (1 KO) na sare moja, ameahidi kulitumia pambano lake la Mei 24,2025 dhidi ya bondia Limbani Lano kutoka Malawi kuonyesha muonekano mpya wa uchezaji sambamba na burudani ya kipekee tofauti na alivyozoeleka huko awali.
Baada ya takribani miezi nane kuwa nje ya ulingo, bondia wa ngumi za kulipwa Tanzania, Twaha Kassimu Rubaha maarufu Twaha Kiduku, ameibuka na kusema ukimya wake ulikuwa ni sehemu ya maandalizi ya kurejea kwa nguvu mpya na kufanyia kazi ushauri na matamanio ya mashabiki ili kuendana mahitaji ya soko la ngumi.
Kiduku ambaye ni bondia kutoka mkoani Morogoro mwenye rekodi ya mapambano 35, akishinda 24 (9 KO), kupigwa 10 (1 KO) na sare moja, ameahidi kulitumia pambano lake la Mei 24,2025 dhidi ya bondia Limbani Lano kutoka Malawi kuonyesha muonekano mpya wa uchezaji sambamba na burudani ya kipekee tofauti na alivyozoeleka huko awali.
Charles Mbwana, mwalimu wa Kiduku, amesema amemuandaa bondia huyo kucheza kwa kiwango cha juu na kuonyesha burudani ya kipekee, akisisitiza kuwa maandalizi ya kumkabili Lano yameshakamilika, huku wakitarajia kuondoka Morogoro Mei 23, kuelekea Dar es Salaam.
Kiduku, bondia mwenye nyota mbili akikamata nafasi ya pili kwenye uzani wa super-middle Tanzania na ya 160 duniani kati ya mabondia 1,773, mara ya mwisho alipanda ulingoni Septemba 24, 2024 alipopambana na Mjerumani, Juergen Doberstein na kupoteza pambano hilo lililofanyika Ujerumani. Ndani ya Tanzania, mara ya mwisho alipanda ulingoni Aprili 24, 2024 alipomtangwa Harpreet Singh raia wa India. Katika pambano hilo la Mei 24, 2025 atacheza katika uzani wa Middleweight (kilo 76).
Kwa upande wa Lano, bondia wa nusu nyota kutoka Malawi, ana rekodi ya mapambano 27, akishinda 8 (4 KO), kupigwa 17 (8 KO) na sare 2. Huyu ni bondia wa nne kwenye uzani wa Light-heavy nchini Malawi huku akishikilia nafasi ya 894 Duniani.
Mei 24, 2025 jumla ya mabondia 30 wataminyana ulingoni katika pambano la Kimataifa la Knockout ya Mama awamu ya nne kwenye viwanja vya Posta, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha pia mabondia mahiri ambao hawajaonekana ulingoni kwa muda mrefu akiwemo Dulla Mbabe, Idd Pialali, Tanzania One, huku pambano kuu likiwa ni bondia Mtanzania, Mchanja Yohana atakayelinda mkanda wake wa WBO Global Flyweight Championship dhidi ya Filemon Ngutenanye kutoka Namibia.