Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba yanunua bao la Yanga

Joseph Kimwaga

Muktasari:

Karibu mwezi mzima walikuwa wanahadithiana bao la ushindi lililofungwa na bwana mdogo mmoja anaitwa Joseph Kimwaga. Simba walikuwa wanaongeza chumvi ili kuwakera tu mashabiki wa Yanga, unajua walikuwa wanasemaje? Eti Yanga kapigwa goli kwa shuti la kutoka Temeke mpaka Buguruni.

KUNA mechi moja kama unaikumbuka ilichezwa Oktoba 2013 pale Taifa baina ya Yanga na Azam kwenye Ligi Kuu Bara na ikamalizika kwa Azam kushinda mabao 3-2. Hiyo mechi iliwapa cha kuongea sana mashabiki wa Simba wanaoishi Dar es Salaam.

Karibu mwezi mzima walikuwa wanahadithiana bao la ushindi lililofungwa na bwana mdogo mmoja anaitwa Joseph Kimwaga. Simba walikuwa wanaongeza chumvi ili kuwakera tu mashabiki wa Yanga, unajua walikuwa wanasemaje? Eti Yanga kapigwa goli kwa shuti la kutoka Temeke mpaka Buguruni.

Yaani wakimaanisha shuti la kufa mtu, basi Yanga wakisikia hizo kejeli wote wananywea, Simba anachukua pointi tatu za kijiweni.

Sasa sikia hii, kipele kimepata mkunaji. Azam imewapa Simba huyo mchezaji ambaye aliinyamazisha Yanga usiku kucha. Msimbazi wamemsainisha mkataba wa mwaka mmoja na Rais wa Simba, Evans Aveva ameithibitishia Mwanaspoti kwamba kila kitu kipo freshi.

Kuanzia juzi Alhamisi viongozi wa Simba walikuwa wakihaha jinsi ya kumalizana na viongozi wa Azam FC kwa ajili ya kunasa sahihi ya mshambuliaji Kimwaga ambaye aliiua Yanga katika msimu huo walipowafunga bao 3-2 katika dakika za lala salama wakati matokeo yao yakiwa ni bao 2-2.

Mechi hiyo iliyochezwa Oktoba 2013 ndiyo ilikuwa ni moja ya mechi zake za mwishoni kwa Kimwaga kucheza mechi za Ligi Kuu Bara kwani mwezi uliofuata mshambuliaji huyo aliumia goti na kulazimika kufanyiwa upasuaji Afrika Kusini.

Baada ya upasuaji huo, Kimwaga amekaa nje ya uwanja mpaka hivi sasa na zaidi tu amecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Friends Rangers iliyochezwa Juni pale Chamazi na kuifungia bao timu yake.

Klabu yake ikaamua apelekwe Simba kwa mkopo ili aweze kupata nafasi ya kucheza kutokana na kikosi chao cha Azam kwa sasa kukamilika kila idara.

MSENEGALI

ATUA SIMBA

Simba bwana, eti wanasema yule straika Msenegali, Papa Niang aliyetua jana Ijumaa amekuja na nguo mpaka za Krismasi.

Mchezaji huyo ambaye ana uhakika mkubwa wa kusajiliwa na Mnyama aliwakosha viongozi wa Simba jana kwenye Uwanja wa Ndege kwani alikuja na lundo la mabegi kana kwamba amehamia Tanzania moja kwa moja.

Lakini viongozi wa Simba waliiambia Mwanaspoti jana kwamba mchezaji huyo ni kifaa na ni uhakika kwamba lazima akipige Msimbazi na ni fundi kwelikweli wa kupachika mabao.

Baada ya kutua Niang alisema: “Nimecheza klabu kubwa Ulaya kwa miaka minane kisha nikaenda barani Asia pia nikacheza klabu kubwa kwa mwaka. Iweje nishindwe kuichezea Simba? Nimecheza timu kubwa na sasa nikuja kufanya kazi kwenye timu kubwa Tanzania, hivyo naamini nitafanya makubwa na kuisaidia Simba.

“Mimi ni straika, mimi ninaweza kufunga mabao na pia ninaweza kutengeneza mabao. Pia ninaweza kucheza nafasi ya mshambuliaji wa pembeni na hivyo sioni kama nitaweza kushindwa kwa sababu nimecheza muda mrefu na nina rekodi nzuri ya ufungaji wa mabao nikitumiwa kwenye nafasi mbalimbali na kwa mifumo tofauti.

“Nimecheza miaka minane Ulaya kabla ya kujiunga na klabu ya Al Shabab SC ya nchini Kuwait na kote nimeshiriki mashindano makubwa na kufanya vizuri. Hivi karibuni kwenye Ligi Kuu ya Kuwait nimefunga mabao manane na nimetengeneza mabao 11 na hii imetokana na mimi kucheza kama straika wa pili yaani nyuma kidogo ya straika anayekuwa mbele lakini ni kwa sababu timu yetu ilikuwa ikicheza sana kwa mfumo wa 4-4-2.

“Hata hivyo sioni kama majaribio ni dili kwangu kwa sababu ninajielewa na ninajua uwezo wangu. Sijui kwanini Simba wanapoteza muda.

“Ninacheza nafasi zote za idara ya ushambuliaji. Kazi itakuwa ni kwa kocha kuamua nicheze wapi lakini kimsingi nitafunga mabao nikiwa kokote.”

Atakaoshindana nao

Niang akifuzu majaribio ambayo atakuwa akifanya Simba kwenye uwanja wa Boko Veterani atakutana na vita kali ya nafasi dhidi ya wachezaji watano wa idara ya ushambuliaji.

Atakaoshindana nao ni Ibrahim Ajibu, Mussa Hassan ‘Mgosi’, Danny Lyanga. Kwenye nafasi za pembeni atakumbana na changamoto kutoka kwa Peter Mwalyanzi pamoja na Simon Sserunkuma.