Simba, Yanga zaibeba Tanzania kuandaa Afcon 2027

Muktasari:
- Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro, amesema idadi kubwa ya mashabiki wa Simba na Yanga na hamasa ndio kigezo moja wapo cha Tanzania kupata fursa ya ufunguzi au fainali ya Michuano Soka Barani Afrika (AFCON) 2027.
SERIKALI imetaja moja ya sababu iliyoipa nafasi Tanzania kuwa moja ya nchi itakayoandaa fainali za mataifa ya Africa (AFCON) kuwa ni Simba na Yanga.
Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro, amesema idadi kubwa ya mashabiki wa Simba na Yanga na hamasa ndio kigezo moja wapo cha Tanzania kupata fursa ya ufunguzi au fainali ya Michuano Soka Barani Afrika (AFCON) 2027.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka mashabiki wa Simba na Yanga kuhamia kuziunga mkono timu za Taifa Ili kutoa hamasa ziweze kufanya vizuri .
“Hamasa ya mpira wa Yanga na Simba imekuwa chachu kubwa na ndio maana CAF wameweka mechi ya ufunguzi wa 'Super League' dhidi ya Al Hilal itakaofanyika Oktoba 20 mwaka huu jijini Dar Es Salaam," amesema Dkt Ndumbaro.
Pamoja na hilo alizitaka Klabu hizo zisibweteke kwenye nafasi za uwakilishi wa mashindano ya kimataifa na kuzitaka zifanye mazoezi zaidi ili kuwa vizuri kwenye michuano hiyo.
Aliongeza "Wajibu wa Serikali na Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tayari tumeleta Afcon Sasa kazi ipo kwa watanzania kuhakikisha wanaunga juhudi za wachezaji wa timu zote kupata sapoti,".
Waziri huyo alisema kuwa wanaendelea kuweka nguvu ya maandalizi ikiwamo ya ujenzi wa viwanja Kwa kuhakikisha vinakamilika mapema na kwa wakati.
Aliwapa wasaa sekta Binafsi kuhakikisha wanajipanga na kuchangamkia fursa hizo pindi timu zitakapowasili nchini zitahitaji huduma mbalimbali ikiwamo chakula, malazi na usafiri.
"Safari bado haijaisha tuna mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya Togo na hii ni muhimu tufuzu WAFCON ,tunataka baada ya kupata nafasi AFCON 2027 ",alibainisha Dkt Ndumbaro.
Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Wallace Karia, alisema kuwa matayarisho yameanza Kwa kuwasilisha mapendekezo ya timu Ili iweze kufanya vizuri.
Amesema Kuwa Tanzania itavaana dhidi ya Ivory Coast katika mchezo wa Afcon utakaofanyika Januari 2024 na kufuatiwa dhidi ya Morocco katika mchezo utakaochezwa Mwaka 2025 yatakuwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Afcon 2027.