Simba yaiwahi Yanga kwa Mkapa

Simba yaiwahi Yanga kwa Mkapa

WAKATI kikosi cha Simba kikiwasili kwa Mkapa saa 11:09 jioni, watani zao Yanga walitia timu dakika 12 baadaye kupitia mlango wa dharula.

Kama ambavyo imekuwa ada pindi timu hizo ziwasilipo kwenye dabi, ndivyo ilivyokuwa muda mfupi kabla ya kikosi hicho cha Wananchi kuwasili.

Makomandoo walijipanga kandokando ya sehemu ambayo gari la timu kubwa  lilipotakiwa kupaki kiasi cha kuzua taharuki.

Baadhi ya mashabiki ambao walikuwa wakikatisha eneo hilo, iliwabidi kusogea ili kuona mastaa wao lakini ilikuwa tofauti kwani alionekana kushuka kocha wa timu hiyo, Nasreddine Nabi na viongozi wengine.

Wachezaji hawakuonekana kushuka na tulipofanya utafiti tukabaini kuwa hakuna mchezaji ambaye alikuwepo ndani.

Bus la nyuma ya lile ambalo wengi waliamini lilikuwa na wachezaji ndilo ambalo lilielezwa kuwa lilikuwa na nyota wa kikosi hicho.

Muda mchache baadaye ndipo shangwe lilipoibuka ndani kwani nyota wa Yanga wakiongozwa na Fiston Mayele walikuwa wakiingia kwa mlango usio rasmi (dharula) ambako imekuwa ikipaki gari la zimamoto.

Mashabiki wa Yanga walishangilia hadi wachezaji wao wapoingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.