Simba yaingia vitani na Azam, Ihefu yampandia dau beki tano

Muktasari:

  • Katika dirisha dogo lililopita Lawi alikuwa anahusishwa na Simba kwenda kusaidiana na beki Henock Inonga na Che Malone Fondoh, huku Keneddy Juma akitajwa kuachwa, lakini mambo yakaenda tofauti.

Baada ya kumkosa katika dirisha dogo la usajili na staa huyo kuwahiwa na Ihefu FC ambayo imetuma ofa Coastal Union ikimtaka Lameck Lawi, Simba imepanda dau kuwania saini ya beki huyo.

Katika dirisha dogo lililopita Lawi alikuwa anahusishwa na Simba kwenda kusaidiana na beki Henock Inonga na Che Malone Fondoh, huku Keneddy Juma akitajwa kuachwa, lakini mambo yakaenda tofauti.

Mwanaspoti imezinasa habari za ndani kutoka Coastal Union kuwa Ihefu FC na Simba zinachuana kuwania saini ya Lawi.

Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya timu zote mbili vimeliambia Mwanaspoti kuwa Ihefu FC wameweka mezani Sh230 milioni kunasa saini ya Lawi ambaye ni beki wa kutumainiwa  Coastal Union.

Ili kuipiku Ihefu, taarifa zinasema Simba imepanda dau kwa kuweka Sh250 milioni ili iweze kukamilisha dili la beki huyo ambaye bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Wagosi wa Kaya.

"Ihefu FC ndio walianza kutuma ofa lakini Simba nao wameingia kwa kuonyesha kumuhitaji mchezaji wetu hivyo tuna ofa mbili mezani," kimesema chanzo hicho.

“Imetumwa ofa ya 230 milioni kwa ajili ya kumpata beki huyo ambaye ni pendekezo la kocha kutokana na mabeki wetu wa kati kupishana mara kwa mara kutokana na kuwa majeruhi, hivyo kocha amesema kuna umuhimu wa kuongeza nguvu eneo hilo."

Mmoja wa viongozi kutoka ndani ya Ihefu: “Tumemfuatilia kwa ukaribu mchezaji huyo na kuridhishwa na uwezo wake anaweza kuwa msaada mkubwa kikosini kwetu msimu ujao endapo ofa yetu itapokewa na kwenda kama tunavyotarajia.”

Chanzo hicho kimesema mazungumzo kati ya timu hizo mbili yanakwenda vizuri na mambo yakiwa tayari wataweka wazi, lakini sasa wanaendelea kupambana ni namna gani wanaweza kufanikisha hilo.

Mwanaspoti lilipomtafuta beki huyo amesema bado ni mali ya Coastal Union kwa sababu ana mkataba hadi 2024.

"Sijajua lolote kuhusiana na ofa zilizopo kunihusu kwani mimi bado ni mchezaji wa Coastal Union kwa mkataba wa mwaka mmoja, hivyo siruhusiwi kufuatwa na timu yoyote. Wanaonihitaji wanatakiwa kufanya mazungumzo na klabu," amesema.

"Hakuna timu imenipigia simu wala kunifuata kwa ajili ya mazungumzo yoyote kuhusiana na kuhitaji huduma yangu. Kama hayo unayosema yana ukweli viongozi watanishirikisha mambo yakiwa tayari yamekamilika."