Simba yafanya usajili wa kushtukiza, Aveva achekelea
Muktasari:
Aveva ameapa kwamba hata kama iwe imesalia sekunde moja lazima wasainishe jembe moja la kigeni.
RAIS wa Simba, Evans Aveva, amewashusha presha mashabiki wa timu hiyo. Amewataka kuacha mchecheto kwani amewahakikishia kwamba wao kama mabosi wa klabu wanajua kila kitu kinachohitajika na lazima wasajili straika wa maana kabla ya usajili kufungwa kesho Jumapili saa 6:00 usiku.
Aveva ambaye anaonekana kujiamini zaidi ameapa kwamba hata kama iwe imesalia sekunde moja lazima wasainishe jembe moja la kigeni. Kiongozi huyo ambaye pia ni mwanachama wa kundi la Friends of Simba alisisitiza kwamba mchezaji watakayemsajili dakika za mwisho si lazima awe Msenegali Pape Abdoulaye au Mmali Makan Dembele bali kuna kifaa kiko sehemu ambacho wanaweza kukishusha na kumaliza kazi mapeema kabisa.
Pape ambaye ni mrefu kuliko mastraika na mabeki wote wa Ligi Kuu nchini, tayari yupo Zanzibar kwenye kambi ya Simba akijifua na kocha Dylan Kerr amesema kwamba atamuangalia kwenye mechi ya leo Jumamosi dhidi ya KMKM kwenye Uwanja wa Amaan. Dembele alitarajiwa kuwasili usiku wa kuamkia leo na ataanza kupasha na Simba mchana ambapo kesho Jumapili ndio atajaribiwa kwenye mechi na Mtibwa itakayochezwa Zanzibar.
USAJILI KUFUNGWA
Mara baada ya kulisogeza mbele dirisha la usajili wa timu za Ligi Kuu Bara mara mbili, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeziambia klabu za Simba na Yanga kuwa inatosha kufanya usajili na wanafunga dirisha hilo kesho Jumapili.
TFF ilitoa siku 10 za usajili wa dharura kati ya tarehe 20-30 ya mwezi huu ambao utaambatana na faini ya Sh 500,000 baada ya kufungwa kwa usajili wa kawaida Agosti 20. Awali dirisha la usajili lilikuwa lifungwe Agosti 6 lakini TFF iliamua kulisogeza mbele kwa wiki mbili zaidi bila sababu za msingi.
Simba bado inapambana na masaa hayo machache yaliyobaki kujinusuru kwa kusajili mtu wa maana atakayeokoa jahazi kwenye fowadi yao. Hata hivyo Yanga na Azam ndizo zinaonekana kunufaika zaidi na usajili wa majira haya baada ya kuwasainisha mastaa kibao wa viwango vya juu pengine kuliko Simba.
Azam imewasainisha Allan Wanga kutoka Kenya, Ramadhan Singano, Ame Ali na Jean Mugiraneza ‘Migi’ wakati Yanga wao wamewasainisha Vincent Bossou kutoka Togo, Thaban Kamusoko na Donald Ngoma kutoka Zimbabwe pamoja na wazawa kadhaa wakiwemo Malimi Busungu na Deus Kaseke.
Simba hiyo inajivunia usajili wa Mohammed Faki, Mwinyi Kazimoto, Peter Mwalyanzi, Mussa Mgosi na Justice Majabvi ambao imewanasa katika usajili huu. Wengine ni kipa Vincent Angban kutoka Ivory Coast na Hamis Kiiza kutoka Uganda.
Mwadui FC ya Shinyanga nayo ilitawala vichwa vya habari vya magazeti mengi baada ya kuwasainisha nyota zaidi ya 10 waliowahi kutamba na timu kubwa nchini.
Timu za Toto African ya Mwanza, Stand United ya Shinyanga na Coastal Union ya Tanga hizo zilikumbana na rungu la faini la Sh 500,000 baada ya kushindwa kuwasilisha usajili wao kabla ya Agosti 20.
SIMBA YAMKOSA KIPA
Simba ilimtolea macho Malimi Busungu, akawatoka akatua zake Yanga. Ikamtangaza kumanasa Laudit Mavugo, naye ikashindikana na kusalia kwao Burundi. Ikaweka bayana kwana imemtema Ivo Mapunda ili kumsajili Mzanzibar, Abdulraham Mohammed kutoka JKU. Sasa unajua kimetokea nini tena, kipa huyo naye ameshindwa kutua Msimbazi.
Kipa huyo alishatangazwa kutua Msimbazi mapema wakati Mohammed Fakhi na Samih Haji Nuhu wakisajiliwa Simba, lakini ikabainika Msimbazi iliingia chaka kwa kumalizana na mchezaji mwenye mkataba kama ilivyokuwa kwa Mavugo.
Ikarudi kujipanga kisha kuingia na gia kubwa baada ya kumsainisha mkataba Vincent Angban yule kipa Mu-Ivory Coast aliyechemsha majaribio yake katika klabu ya Azam. Baada ya kujiridhisha ikarudi tena Zenji na kumalizana na JKU ili kumchukua Mohammed, lakini dili hilo limekwama kwa mara nyingine. Safari hii inaelezwa kuwa kocha Dylan Kerr amemkataa kipa huyo. Amedai hana hadhi ya kuidakia Simba.
Lakini kocha wa JKU, Malale Hamsini aliliambia Mwanaspoti, Simba imemkosa kipa huyo baada ya mtu aliyekuwa aje kumalizana nao, kushindwa kutua wakati mambo yalishakamilika kwa asilimia kubwa.