Vurugu mchezo wa Stand, Fountain DC Mtatiro aingilia kati

Muktasari:
- Baada ya bao la tatu la Fountain Gate lililofungwa dakika ya 82, mashabiki wa Stand wakaanzisha vurugu kwa kutoridhishwa na uamuzi ya refa.
Baada ya bao la tatu la Fountain Gate lililofungwa dakika ya 82 na Mudrick Gonda katika mechi ya play off ya kwanza, mashabiki wa Stand United 'Chama la Wana' waanzisha vurugu kwa kurusha mawe na makopo kwa wachezaji wa Fountain Gate waliokuwa benchi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo kwenye Uwanja wa Kambarage, wenyeji Chama la Wana walipasuka kwa mabao 3-1.
Mechi ya marudiano kwa timu hizo utapigwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara, ambapo mshindi wa jumla kama atakuwa ni Stand United itapanda daraja na Fountain itashuka daraja.
Iwapo Fountain itashinda itasalia Ligi Kuu na kuizuia Stand kurejea katila Ligi hiyo ikishindwa kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizopanda daraja moja kwa moja kutoka Ligi ya Championship.
Kutokana na tukio hilo lililotokea leo Julai 04, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro ameingilia kati kwa kuwatuliza mashabiki hao kwa kuzuia vurugu hizo kwa kushirikiana na Kamati ya Usalama.
“Bahati mbaya zaidi tumepoteza mchezo wa nyumbani kwa mabao 3-1 ambao tungeutumia kwa faida, lakini bado kuna mechi ya pili vijana wa Stand wakipambana wanaweza kupata ushindi ugenini," amesema Mtatiro.
Naye Kocha wa Fountain Gate Mohammed Laizer ameeleza mbinu walizotumia zimewapa faida kwa kupata ushindi ugenini baada ya kutambua madhaifu ya Stand.
“Stand ni wazuri kwa upande wa pembeni wa uwanja tulipotambua hilo, tuliangalia namna ya kuziba hiyo mianya ili kutoka na ushindi," amesema Laizer.
Kwa kocha wa Stand United, Juma Masoud amesema bado wana matumaini ya kupata ushindi kwa kuwa, bado wana mechi nyingine ya ugenini na watajipanga zaidi na kurekebisha makosa.
“Kama Fountain wamepata ushindi ugenini, nasi tuna imani ya kupata ushindi ugenini, cha muhimu tutarekebisha pale tulipokosea kwa ajili ya mchezo wa pili,” amesema Masoud.