Simba yaenda mapumziko kifua mbele, Ajibu hakabiki

DAKIKA 45 za mchezo wa kombe la Azam Sports Federatio Cup (ASFC) kati ya African Lyon na Simba zimemalizika Simba wakiongoza kwa bao 2-0.

Imewachukua dakika 10 Simba kuandika bao la kwanza lililofungwa kwa kichwa na Ibrahim Ajibu akimalizia kona kiki ya Rally Bwalya.

Lango la African Lyon liliendelwa kuwa hatarini kutokana na mashambuliZi ya mara kwa mara waliyoyafanya Simba lakini mabeki wa Lyon walijitahidi kutibua mipango ya Simba.

Eneo la beki wa kushoto kwa Lyon alipokuwa akicheza Paschal Kibandula lilionekana kuwa njia ya Simba kutengenezea mipango yake wakimtumia winga Hassan Dilunga.

Dakika ya 19 Lyon walitengeneza shambulizi langoni kwa Simba ambalo hata hivyo halikuzaa matunda kwani mshambuliaji Sadi kipanga alipiga kiki iliyopaa juu.

Simba walipata penati dakika ya 21 baada ya Chikwende kukwatuliwa ndani ya boksi la 18 na sekunde kadhaa baadae ilipigwa na Kagere na kwenda nje.

Ibrahim Ajibu yule yule aliyefunga bao la kwanza, dakika ya 44 aliwainua tena mashabiki wa Simba baada ya kufunga bao akipiga mpira uliopanguliwa na kipa wa Lyon Bwanaheri Abdallah akiokoa kiki kali iliyopigwa na Bwalya.

Pamoja na kwamba wameenda mapumziko ya kipindi cha kwanza wakiongoza kwa bao 2-0 lakini Simba watajilaumu kwa kushindwa kufunga kwenye nafasi za wazi walizopata hususani Kagere, Chikwende, Dilunga  na Bwalya.

Kiungo wa Lyon Saidi Mtikila alionekana kuwa bora zaidi eneo la kati  licha  ya timu yake kwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa bao 2-0.