Simba kuendeleza utetezi Kombe la FA

Dar es Salaam. Baada ya kuicha Al Ahly kwa bao 1-0 katika mchezo wa Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba inarejea nyumbani kuendeleza heshima ikiivaa African Lyon katika raundi ya nne ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam.

Mchezo huo wa heshima ikijaribu pia kuendeleza kampeni za kutetea

kombe hilo, utafanyika kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Saal, kuanzia saa 1 usiku.

Simba imekuwa na rekodi nzuri dhidi ya African Lyon ambapo katika mechi 10 za mashindano ambazo wamewahi kukutana, imeibuka na ushindi mara tisa na imepoteza mchezo mmoja tu.

Hata hivyo hilo halipaswi kuwafanya waingie leo wakiwa wameidharau African Lyon kwani wamekuwa na historia isiyovutia ya kukutana na vipigo vya kushtua kutoka kwa timu za madaraja ya chini pindi inapokutana nazo kwenye mashindano hayo.

Msimu wa 2015/2016, Simba ilitolewa katika hatua ya robo fainali na Coastal Union ambayo ilishuka daraja na msimu wa 2017/2018 ilitolewa na Green Warriors katika hatua ya 32 bora huku msimu wa 2018/2019 ikitupwa nje na timu ya Mashujaa FC.

Wakati Simba ikiingia kwenye mechi hiyo ikiwa katika hali nzuri

kisaikolojia baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly,

Jumanne iliyopita huku ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, Lyon yenyewe imekuwa na mwendo wa kusuasua kwenye Ligi Daraja la Kwanza ikiwa inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa kundi A ikiwa na pointi 10.

Huenda kukawa na mabadiliko makubwa katika kikosi cha kwanza cha Simba leo ambapo baadhi ya wachezaji wanaosotea benchi wanaweza kuanzishwa ili kuwapa mwanya wa kupumzika wengine ambao wametoka kutumika katika mechi za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Lakini pia uamuzi huo unaweza unaweza kulenga kutowaweka wachezaji wa Simba katika hatari ya kupata majeraha ukizingatia wanakabiliwa na ratiba ngumu ya mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo watakabiliana na El Merrikh ya Sudan kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini lakini pia wanakabiliwa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya JKT Tanzania.

Michezo mingine ya mashindano hayo itachezwa kesho.